
Unguja. Serikali imesema Sh38 bilioni zimetumika kuwalipa fidia wananchi waliopitiwa na miradi mbalimbali ya maendeleo katika maeneo yao kisiwani hapa.
Kauli hiyo imetolewa leo Jumatatu, Machi 2, 2026, na Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed, katika mkutano na waandishi wa habari kuelezea mafanikio ya siku 100 za Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo, Rahaleo Mjini, Unguja.
Waziri Khalid amesema Serikali inalipa fidia wananchi wake kwa kuzingatia uhalisia wa thamani au vipande baada ya kufanyiwa tathmini.
Pia amesema Serikali inatoa nafasi kwa wananchi ambao hawajaridhika na malipo kuwasilisha malalamiko yao, na yanapofanyiwa kazi, endapo kugundulika kwamba anayestahiki kulipwa, anapewa fedha yake iliyopungua.
“Sh38 bilioni zimelipwa fidia, kati ya hizo, Sh12 bilioni wamelipwa wananchi waliopitiwa na mradi wa uwanja wa ndege kisiwani Pemba. Katika kipindi hiki tunazingatia zaidi ulipaji wa fidia kabla ya kuanza mradi,” amesema Dk Khalid.
Amewataka wananchi wasiwe na hofu kwani Serikali haina lengo la kumnyima mtu yoyote haki yake, lakini ametoa wito kwa wananchi kuacha kujenga katika maeneo ya hifadhi za barabara ili kuepuka kuipa hasara Serikali.
“Kama Serikali ingesema inafuata sheria katika kulipa fidia, wengi wao wasingelistahiki kulipwa kwani wapo katika hifadhi ya barabara,” amesema.
Mbali na hilo, Waziri Khalid amesema wizara hiyo imefanikiwa kukamata watu waliofanya makosa ya usalama barabarani 1,711 na kukusanya Sh1.9 milioni kupitia faini walizotozwa wenye makosa hayo.
Amesema Serikali haitozi faini hizo kwa kuwakomoa waendesha vyombo vya moto, badala yake, inahitaji wananchi watii sheria bila kushurutishwa.
Hivyo, ametoa wito kwa madereva kuacha kuendesha mwendo kasi barabarani kwa sababu wanasababisha ajali zisizo za lazima kwa wengine.
Vilevile, Waziri huyo amewataka wananchi ambao hawajapitiwa na miradi ya barabara wasiwe na wasiwasi, kwani wapo katika mpango wa ujenzi na wanapaswa kuwa tayari.
Amesema katika awamu ya kwanza iliyopita, wizara ilifanikiwa kujenga kilomita 1,084 za barabara, na katika kipindi hiki ina mpango wa kujenga barabara kuu kilomita 523, ambapo hadi sasa kilomita 83.3 zimeanza kujengwa katika kipindi cha siku 100.
Amesema Serikali imeshafanya maandalizi ya ujenzi wa barabara hizo zinazolenga kuimarisha shughuli za uchumi kwa wananchi.
Katika hatua nyingine, Dk Khalid amesema wakati ujenzi wa miundombinu ukiimarishwa zaidi, Serikali imejipanga kudhibiti usalama barabarani na imeshatoa mafunzo hayo kwa madereva 885.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar, Salum Ramadhani Abdallah, ametaka wizara kuendelea kuwa na ushirikiano na vyombo vya habari katika kuelezea wananchi mafanikio yaliyopatikana.