Trump alisema Urusi iko katika matatizo makubwa ya kiuchumi kutokana na vita na kwamba msaada wa Umoja wa Ulaya unaweza kuiwezesha Ukraine kupigania na kushinda, ikijumuisha kurejesha Rasi ya Crimea ambayo Moscow iliinyakua tangu mwaka 2014. Kauli hiyo, ikiwa itatekelezwa, itamaanisha Kyiv kulazimika kuwafurusha wanajeshi wa Urusi kutoka takribani asilimia 20 ya ardhi yake.

Awali, Trump alikuwa amependekeza Ukraine ifikirie kutoa baadhi ya maeneo ili kupata amani, mbinu ambayo imekosolewa vikali Kyiv iliyoashiria uwezekano wa makubaliano ya nyuma ya pazia ya kutambua maeneo yaliyochukuliwa na Urusi. Ndiyo maana msimamo wake wa sasa unachukuliwa kama “mabadiliko makubwa,” kwa mujibu wa Rais Volodymyr Zelenskiy.

Zelenskiy aliliambia Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba China inaweza kuishinikiza Urusi kusitisha vita, sambamba na wito wa Marekani kwa Beijing kuacha kununua mafuta ya Urusi. Aliongeza katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Fox News, kwamba mitazamo ya Kyiv na Washington sasa iko karibu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.

“Trump ndiye pekee anayeweza kubadili mambo. Ikiwa ataamua kwa uhakika kuhusu Ukraine, naona sasa yuko karibu zaidi na hali hii, na ndiyo maana nasema hivyo. Kati ya viongozi tulionao duniani kwa sasa, ni wachache tu wanaoweza kuleta mabadiliko makubwa, lakini Trump ndiye yuko karibu zaidi kufanya hivyo.”

Kaja Kallas asifu kauli za Donald Trump

 Kaja Kallas
Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja KallasPicha: Nicolas Tucat/AFP

Mkuu wa sera za nje wa Umoja wa Ulaya, Kaja Kallas, alisifu kauli za Trump akisema ni mara ya kwanza kauli kali kama hizo zimetolewa “katika muundo wa aina hii.” Pia, Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza Yvette Cooper alisema taifa lake liko “tayari kuchukua hatua” baada ya Trump kuzitaka nchi wanachama wa NATO kuzidungua ndege za Urusi zinazoingia katika anga za muungano huo, akilaani hatua za Moscow kama “za kichokozi na zisizo na uwajibikaji.”

Pamoja na maneno hayo makali, wachambuzi wanasema hakuna dalili kwamba sera ya Marekani itabadilika haraka. Hakuna uamuzi mpya wa vikwazo vizito dhidi ya Moscow kama alivyoomba Zelenskiy, na kauli pekee ya Trump yenye uzito ilikuwa ni kuendelea kusambaza silaha kwa NATO kupitia mfumo mpya wa manunuzi ya pamoja.

Ikijibu kauli za Trump, ikulu ya Kremlin imesema haina budi kuendelea na “operesheni maalum ya kijeshi” kufikia malengo ya Rais Vladimir Putin. Msemaji wake Dmitry Peskov alipuuza kauli ya Trump kwamba Urusi ni “nguvu ya soda.” Hata hivyo, amekiri kuwa uchumi wa Urusi unakabiliwa na changamoto katika sekta mbalimbali licha ya kudumisha “uthabiti wa uchumi mdogo.”

Aidha, Kremlin ilitoa tathmini ya kukatisha tamaa kuhusu jitihada za kurekebisha uhusiano na Marekani, ikisema mchakato huo umetoa “matokeo karibu na sifuri.” Peskov aliongeza kuwa jitihada za kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kidiplomasia kati ya Washington na Moscow zimesalia “za kusuasua sana.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *