China imeonya kwamba kuendelea kwa vita dhidi ya Iran kunaweza kuzidisha zaidi mgogoro unaoendelea katika eneo la Asia Magharibi.

Shirika la Habari la Mehr limeandika kuwa, Waziri wa Mambo ya Nje wa China, Wang Yi, akijibu mawasiliano ya simu kutoka kwa waziri wa mambo ya nje wa utawala wa Kizayuni, amesema kwamba migogoro na tofauti za kikanda na kimataifa lazima zipatiwe suluhisho kupitia njia za kidiplomasia.

Wang Yi amesisitiza kwamba pande zote zinazohusika zinapaswa kuzingatia kwa makini Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Ameongeza kuwa licha ya hatua zilizokuwa zimepigwa hivi karibuni kuelekea suluhisho la kidiplomasia kuhusu suala la nyuklia la Iran, mashambulizi ya karibuni yamevuruga mchakato huo.

Amebainisha kuwa matumizi ya nguvu hayawezi kutatua matatizo yoyote, na akaonya kuhusu matokeo hatari na magumu yanayoweza kusababishwa na hatua za kijeshi za kiholela za utawala huo.

Waziri huyo wa China ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mapigano na akahimiza juhudi za pamoja ili kuzuia kuongezeka kwa mvutano. Amebainisha kuwa kuendelea kwa uhasama kunaweza kupanua mgogoro na kuongeza hali ya kukosekana kwa utulivu katika kanda.

Pia amesema kwa mara nyingine kwamba China iko tayari  kuchukua jukumu amilifu katika kupunguza mvutano na kurejesha utulivu katika eneo la Asia Magharibi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *