Msimamizi maalum wa Umoja wa Mataifa (UN), Gina Romero ameisifu Tanzania kwa kuunda tume huru ya uchunguzi ya matukio ya Oktoba 29, 2025, akisema ni uthibitisho wa kujali haki za binadamu. Romero ametoa kauli hiyo Geneva nchini Uswisi Machi 12, alipofanya majumuisho ya mada kuhusu ukweli na uwajibikaji katika uchaguzi mkuu wa 2025 nchini Tanzania.

Gina ameongeza kuwa tume hiyo, inayoongozwa na Jaji Mkuu Mstaafu, Mohamed Chande Othman, ni ishara nzuri ya Tanzania kushughulikia matukio ya Oktoba 29 kwa uwazi na uhuru. Jaji Chande amesifiwa pia na Kamishna wa Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa (UNHRC), Volker Turk, kutokana na uadilifu na ueledi wake, baada ya kushughulikia uchunguzi wa mauaji holela El Fasher, nchini Sudan, na ajali ya ndege iliyomuua Katibu Mkuu wa UN, Dag Hammarskjöld.

Hata hivyo, kauli hizo za UN zimekuja wakati taasisi za Amnesty International na Human Rights Watch zikitoa ripoti zinazodai matumizi makubwa ya nguvu katika kudhibiti vurugu za uchaguzi. Serikali ya Tanzania ilipinga madai hayo, ikisema ripoti hizo hazina usawa, hazijachambua matukio yote, na hazijazingatia mchango wa vyombo vya usalama katika kulinda amani na utawala wa sheria.

Serikali pia ilisisitiza kuwa mitandao ya kijamii ilitumika kueneza chuki, uchochezi na kauli za kihaini kutoka kwa baadhi ya wanasiasa na taasisi za kiraia ndani na nje ya nchi. Tanzania iliomba AI na HRW ziweke wazi kiwango cha nguvu kilichotumika, ili ripoti zao ziwe na ukweli, zisizo na upendeleo wa kisiasa na ziwe huru kwa pande zote.

#AzamTVUpdates
Mhariri | John Mbalamwezi

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *