
Nchini Ethiopia, angalau watu 102 wamefariki kufuatia maporomoko ya udongo yaliyosababishwa na mvua kubwa ambayo imekuwa ikikumba eneo la Gamo kusini mwa nchi tangu mwanzoni mwa wiki. Hii ni idadi ya awali iliyotolewa na mamlaka ya ndani, ambayo imerekebisha takwimu zao mara kwa mara katika siku za hivi karibuni. Bunge la Ethiopia limetangaza siku tatu za maombolezo ya kitaifa, kuanzia leo Jumamosi, Machi 14. Shughuli za utafutaji na uokoaji bado zinaendelea.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Takriban watu 100 wamefariki, nyumba 190 zimeharibiwa, na karibu watu 3,500 wamehamishwa. Mamlaka katika eneo la Gamo, iliyonukuliwa na vyombo vya habari vya Ethiopia, inabainisha kwamba utafutaji unaendelea, kwani watu wengi bado hawajulikani walipo baada ya maporomoko makubwa ya udongo yaliyotokea usiku wa Jumanne, Machi 10 kuamkia Jumatano, Machi 11, kufuatia mvua kubwa iliyonyesha kwa siku kadhaa kusini mwa Ethiopia.
Zikiwa zimejaa maji, nyanda za juu za milimani za wilaya ya Gacho Baba katika eneo la Gamo zilianguka. Barabara zilifunikwa na matope na vifusi, na kufanya wafanyakazi wa uokoaji kupeleka mitambo mikubwa kujaribu kuwatafuta waathiriwa. Mamlaka inawaonya wakazi kuhusu uwezekano wa maporomoko zaidi ya udongo.
Mvua kubwa pia inaikumba Kenya
Katika nchi jirani ya Kenya, mvua kubwa katika siku za hivi karibuni pia zimesababisha vifo vya watu wasiopungua 40 na zaidi ya 2,000 kuhama makazi yao. Hali hii imezidishwa, kulingana na tafiti kadhaa za kisayansi, na mabadiliko ya hali ya hewa yanayosababishwa na shughuli za binadamu.
Mnamo mwezi Julai 2024, maporomoko ya udongo katika eneo la karibu la Geze Gofa kusini mwa Ethiopia yaliwaua watu 229.