
Chombo kimoja cha habari cha Magharibi kimekiri kwamba nchi za Ghuba ya Uajemi zimechoshwa na vita dhidi ya Iran na zinaamini kuwa Marekani haina mkakati wowote katika vita hivi.
Bloomberg imesema katika ripoti yake ya uchambuzi kwamba nchi wanachama wa Baraza la Ushirikiano la Ghuba ya Uajemi zimebadili msimamo wao kuhusu usalama wa kikanda. Kikiashiria hali ya wasiwasi inayoendelea kuongezeka katika miji mikuu ya nchi za Kiarabu, chombo hiki cha habari cha Marekani kimeandika kuwa, nchi hizo zimechoshwa na siasa za kuchochea vita na kutokuwepo uthabiti katika siasa za Marekani kuhusu Iran.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, viongozi wa Ghuba ya Uajemi wanahoji faraghani kuhusu thamani ya kimkakati ya kuwa wenyeji wa kambi za kijeshi za Marekani katika eneo. Uchambuzi wa Bloomberg unasema nchi hizi zinaamini kuwa uwepo wa kambi hizi unaziweka kwenye mstari wa mbele wa mivutano inayoweza kutokea badala ya kuzidhaminia usalama. Chanzo kinachofahamu vizuri suala hilo kimeiambia Bloomberg kwamba, “wasiwasi mkubwa ni kwamba ikiwa mzozo mkubwa zaidi utaibuka, Marekani itawakimbia washirika wake wakati udhibiti wa Lango-Bahari la Hormuz ni muhimu.”
Kukata tamaa kwa nchi hizo za Kiarabu katika vita dhidi ya Iran kunakuja wakati ambapo Waziri wa Mambo ya Nje wa Oman, Badr Al-Busaidy, ameelezea mashambulizi ya Iran kwenye kambi za kijeshi za Marekani katika miji kama vile Dubai, Manama na Doha kuwa “chaguo pekee la kimantiki” katika kukabiliana na mashambulizi ya Marekani na Israel. Anaamini kuwa, hatua ya Iran ya kulenga vituo vya Marekani katika Mashariki ya Kati ni jibu la kimantiki kwa uchokozi wa Washington na Tel Aviv.