
Kikosi cha Wanamaji la Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (IRGC) mapema leo Jumanne kimefanya operesheni nne dhidi ya shabaha za magaidi wa Kimarekani na Israel na kutoa vipigo vikali ikiwa ni sehemu ya wimbi la 88 la Operesheni Ahadi ya Kweli-4.
Idara ya Uhusiano wa Umma ya IRGC imetangaza kuwa, wanajeshi wa majini wa jeshi hilo wamefanya mashambulizi makali dhidi ya maeneo mbalimbali ya adui.
Taarifa ya IRGC imeeleza kuwa, meli ya makontena ya utawala wa Israel, kwa jina Express Halfon, imepigwa na makombora ya balestiki katika maji ya kati ya Ghuba ya Uajemi.
Katika oparesheni ya pili, kikosi cha majini cha Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu kimeshambulia na kulenga kwa usahihi maficho ya wanajeshi wa Marekani kwenye ufukwe wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE), ambako walikuwa wamejificha nje ya kambi za kijeshi wakihofia makombora angamizi ya Iran. Maficho hayo yameharibiwa kwa droni za vilipuzi.
Taarifa hiyo imesema kwamba Jeshi la Wanamaji la IRGC pia limeharibu mfumo wa kukabiliana na ndege zisizo na rubani wa Kikosi cha Tano cha Marekani ambao ulikuwa umejificha nje ya kambi yao karibu na uwanja wa ndege wa Manama huko Bahrain, na kwamba rada mbili za tahadhari ya mapema katika kambi ya magadi wa Marekani ya “Jaber al-Ahmad” nchini Kuwait, zimepigwa na droni.
Taarifa ya IRGC imesisitiza kuwa Mlango Bahari wa Hormuz unasimamiwa kikamilifu na kwa uthabiti na wanajeshi wake.
Wimbi la 88 la Operesheni Ahadi ya Kweli 4 ni la hivi karibuni katika mfululizo wa mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Iran yanayofanyika karibu kila siku tangu Marekani na Israel zilipoanzisha vita vya uchokozi dhidi ya Iran bila sababu yoyote, mnamo Februari 28.