
Songwe. Wachimbaji wadogo zaidi ya 100 wa dhahabu katika Kijiji cha Patamela, Kata ya Saza, Wilaya ya Songwe, wameandamana hadi Ofisi ya Mkuu wa Wilaya wakiiomba Serikali iingilie kati mgogoro wa ardhi unaoendelea kati yao na mwekezaji kuhusu umiliki wa eneo la uchimbaji madini.
Wachimbaji hao wanadai wamekuwa wakilitumia eneo hilo kwa muda mrefu kama chanzo chao kikuu cha kipato, huku wakieleza kuwa mwekezaji aliwahi kuonesha nia ya kuachia leseni ili kuwawezesha kuendelea na shughuli zao.
Wakizungumza na Mwananchi Digital, leo Aprili 2, 2026 wachimbaji hao wamesema wameamua kuandamana kutokana na kupoteza imani kwa uongozi wa kijiji, wakidai haujawashirikisha katika vikao muhimu vya mazungumzo na mwekezaji.
Aidha, wamedai kuwepo kwa dalili za kupinduliwa kwa makubaliano ya awali, hali inayozua hofu kuhusu hatima ya eneo hilo.
Mchimbaji wa kijiji hicho, Salumu Muhamed, amesema kwa sasa mwekezaji anamiliki maeneo mengi ya uchimbaji, jambo linalowaacha wachimbaji wadogo bila sehemu ya kufanyia kazi.
“Tunashangaa kwa nini uongozi wa kijiji na kamati ya ardhi wanashindwa kutupatia eneo la kuchimba wakati tumekaa hapa kwa muda mrefu. Hii imekuwa kikwazo kikubwa kwa vijana wengi wanaotegemea uchimbaji kama ajira,” amesema.
Kwa upande wake, Bahati Mwarabu ameutuhumu uongozi wa kijiji kwa kujinufaisha na eneo hilo, akidai hali hiyo imewaacha vijana wengi bila ajira licha ya kuwepo maeneo ya uchimbaji.
“Kila eneo unaloelekezwa unaambiwa ni la mwekezaji. Tunamuomba Rais Samia Suluhu Hassan atusaidie kupata maeneo ya kufanya shughuli za uchimbaji,” amesema.
Naye Salumu Mubisa amesema ukosefu wa uwazi katika mazungumzo kati ya wachimbaji na uongozi wa kijiji umeongeza sintofahamu na wasiwasi miongoni mwao.
Akizungumza kwa niaba ya uongozi wa kijiji, Diwani wa Kata ya Saza, Raphael Mzumbwe, amesema mazungumzo na mwekezaji bado yanaendelea kwa lengo la kupata suluhu itakayozingatia maslahi ya pande zote.
Amesema kijiji kina dhamira ya kuhakikisha wachimbaji wadogo wanapata eneo la kufanyia shughuli zao endapo mwekezaji ataridhia kuliachia.
“Mazungumzo na mwekezaji yamekuwa yakiendelea tangu Julai 27, 2025, kwa lengo la kuhakikisha wananchi wanapatiwa eneo la kuendelea na shughuli za uchimbaji,” amesema.
Ofisa Madini Mkoa wa Songwe, Mhandisi Abdurahman Birandu, amekiri kuwepo kwa changamoto ya ukosefu wa imani kati ya wachimbaji na uongozi wa kijiji, hali inayochangia mvutano huo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Songwe, Fadhili Nkurlu, amesema ofisi yake imepokea malalamiko hayo na kuahidi kukutana na mwekezaji, ili kutafuta suluhisho ya kudumu itakayowezesha wachimbaji kupata eneo la kufanyia kazi.
Amesisitiza kuwa Serikali itaendelea kusimamia mazungumzo hayo, ili kuhakikisha haki inatendeka kwa pande zote.