
KOCHA Msaidizi wa Chipukizi inayoshiriki Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) kutokea kisiwani Pemba, Mzee Ali Abdallah amesema kwa usajili waliofanya dirisha dogo mismu huu wameanza vizuri mzunguko wa pili na matarajio ni makubwa mwisho wa msimu.
Chipukizi iliuanza msimu huu kwa matumaini kutokana na usajili iliyoufanya dirisha kubwa, lakini malengo hayo hayakutimia, hivyo wakajikuta wanaanza upya mzunguko wa pili.
Akizungumza na Mwanaspoti, kocha Mzee amesema matarajio ya klabu hayakufikiwa vile ambavyo walitaka kutokana na kushindwa kufanya vizuri.
“Baada ya benchi la ufundi kubaini upungufu huo, tuliwasilisha kwa uongozi, nawashukuru kwa kukubali matakwa ambayo yanaenda kukidhi matamanio ya klabu,” amesema.
Kocha Mzee amesema kutokana na usajili uliofanywa dirisha dogo msimu huu, wameanza vizuri na wana matarajio makubwa kutoka kwao na timu italeta upinzani kwa wengine.
Alifafanua, benchi la ufundi la timu hiyo lina matarajio na matumaini ya kusalia kwenye ligi hiyo kwa msimu ujao licha kuanza vibaya na imeanza mazoezi ya kuikabili Mwembe Makumbi na nyingine zijazo kuhakikisha pointi tatu zinabaki nyumbani.
Pia, amesema wanauona usajili huo kuwalipa mzunguko wa pili, hivyo mashabiki wategemee kuiona Chipukizi mpya na yenye ushindani.
Kocha huyo amesema michezo ya Kombe la FA inayoendelea kuchezwa Kanda ya Pemba, wanatumia kama sehemu ya mazoezi ya kujinoa kwa ajili ya Ligi Kuu.
Kocha huyo ametoa wito kwa mashabiki wa timu hiyo kujitokeza uwanjani inapocheza kwa ajili ya kutoa hamasa ya kufanya vizuri.
Chipukizi ipo nafasi ya 12 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Zanzibar, ikivuna pointi 24 kwenye mechi 20 ilizocheza.