Morogoro. Hali ya huzuni, simanzi na sintofahamu imetawala miongoni mwa waathirika wa mafuriko wilayani Mvomero, mkoani Morogoro, huku baadhi yao wakieleza kupoteza kila walichokuwa nacho baada ya mvua kubwa kunyesha kwa nyakati tofauti.
Mvua hizo zilizonyesha Februari 16, 17 na 19, pamoja na Machi 1, 2026, zilisababisha mafuriko yaliyobomoa nyumba, kuharibu mali na kuwaacha mamia ya wananchi bila makazi.
Katika hatua za dharura, baadhi ya waathirika wamehifadhiwa katika shule za msingi Kichangani na Kilimanjaro, ambako wamekuwa wakiishi kwa zaidi ya miezi miwili huku wakikabiliwa na uhaba wa mahitaji muhimu.
Miongoni mwa waathirika ni Tabia Faraji (60), mkazi wa Kitongoji cha Sokoni, Kijiji cha Kichangani, ambaye alishindwa kujizuia kulia aliposhuhudia viongozi wakifika kambini hapo kutoa msaada.
“Nimepoteza kila kitu. Nyumba zangu zote nne zimebomoka, chakula, vyombo, nguo na hata vifaa vya shule vya watoto vimesombwa na maji. Hii nguo niliyonayo nimepewa na mtu mwema,” amesema kwa huzuni.
Baadhi ya wananchi waliokumbwa na mafuriko wakihifadhiwa katika kambi ya muda katika Shule ya Msingi Kilimanjaro, kijiji cha Kichangani wilayani Mvomero, wakisubiri msaada wa kibinadamu baada ya kupoteza makazi yao. Picha na Juma Mtanda
Tabia, anayelea watoto wanne yatima, amesema kwa sasa hana makazi wala uhakika wa maisha ya kesho, akiomba msaada kutoka Serikalini na kwa wadau ili aweze kuanza upya.
Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada wa sukari kilo 5,000 zenye thamani ya Sh14 milioni, Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, Profesa Kenneth Bengesi, amesema taasisi hiyo imeguswa na athari za janga hilo.
“Sisi kama wadau wa Bonde la Mtibwa tumeona ni vyema kushiriki kuwafariji wananchi. Huu ni msaada mdogo, lakini tunaamini utawasaidia wakati Serikali ikiendelea kutafuta suluhisho la kudumu,” alisema.
Kwa upande wake, mkazi wa Msufini, Kibwana Kondo, amesema hofu kubwa waliyonayo ni hatma ya maisha yao baada ya kuondoka kambini.
“Swali kubwa ni tutakwenda wapi? Nyumba zetu zimebomoka. Tunaomba Serikali itupatie maeneo salama ya kuishi na hata mashamba kwa kuwa sisi ni wakulima,” alisema.
Ameongeza kuwa licha ya misaada ya chakula, bado wanakabiliwa na changamoto ya huduma za afya kutokana na uhaba wa dawa katika vituo vya afya.
Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Sarah Msafiri, alisema ofisi yake imeanza kutoa misaada ya dharura ikiwemo mafuta ya kula, dagaa, chumvi na mahitaji mengine yenye thamani ya Sh5 milioni.
Amesema atalifikisha suala hilo katika Ofisi ya Waziri Mkuu ili kutafuta suluhisho la kudumu, hususan kudhibiti mafuriko ya Mto Mbulumi.
“Lazima tutafute suluhisho la kudumu. Hatuwezi kuruhusu wananchi kuendelea kuathirika kila mwaka. Tutatafuta pia maeneo salama ya makazi,” alisema.
Diwani wa Kata ya Muhonda, Rashid Juma, amesema jumla ya kaya 1,830 zimeathirika katika kata za Muhonda na Sungaji kutokana na mvua hizo.
Amesema baadhi ya waathirika wamehifadhiwa kambini huku wengine wakikimbilia kwa ndugu na majirani.
“Katika Shule ya Msingi Kichangani kuna wananchi 55 na Kilimanjaro kuna 16 ambao hawakuwa na pa kwenda kabisa,” alisema.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu tayari imetoa msaada wa mahindi tani 79, maharage tani 23 na mablanketi 300, lakini bado mahitaji ni makubwa.
Wanafunzi ni miongoni mwa walioathirika zaidi. Salha Juma (17), mwanafunzi wa kidato cha tatu, alisema wamepoteza vifaa vyote vya shule.
“Tunaomba tusaidiwe madaftari, sare na mahitaji ya wasichana kama taulo za kike. Wazazi wetu wamepoteza kila kitu,” alisema.
Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari Tanzania, Profesa Kenneth Bengesi (kulia), akimkabidhi Mbunge wa Jimbo la Mvomero, Sarah Msafiri, sehemu ya msaada wa sukari kilo 5,000 kwa ajili ya waathirika wa mafuriko wilayani humo.Picha na Juma Mtanda.
Wananchi hao wameiomba Serikali kuchukua hatua za haraka na za kudumu, ikiwemo kujenga kingo za Mto Mbulumi au kuwahamisha kabisa kutoka maeneo hatarishi.
Kwa sasa, matumaini yao yamebaki kwa Serikali na wadau mbalimbali kuendelea kuwasaidia ili waweze kurejea katika maisha yao ya kawaida baada ya janga hilo.