
Dar es Salaam. Tume ya kuchunguza matukio ya uvunjifu wa amani ya wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025 imebaini kuwa vifo vilivyotokana na ghasia siku hiyo ni 518.
Kutokana na mazingira ya ghasia na madai ya baadhi ya mashahidi idadi hiyo ya vifo iliyobainishwa na Tume inaweza kubadilika kutokana na uwezekano wa kuwepo kwa baadhi ya ndugu waliozika maiti za wapendwa zao bila kufikisha kwenye vituo vya kutolea huduma za afya au hawakupata furasa kufika mbele ya tume.
Pia, amesema inawezekana kulikuwa na majeruhi waliamua kutibiwa nje ya mfumo rasmi na wakafariki dunia bila taarifa zao kufikishwa panapostahili.
Jaji Chande amesema tume imepokea ushahidi na madai kuhusu watu kupotea au kutopatikana tangu uchaguzi mkuu kwa kuzingatia hilo, idadi hiyo ya vifo 518 inaweza kuwa si kauli ya mwisho ya tume.
Akiwasilisha ripoti ya tume hiyo Aprili 23, 2026 Mwenyekiti wake, Jaji Othman Chande amesema idadi hiyo ya vifo wanaume ni 490 sawa na asilimia 94.7, wanawake ni 28 sawa na asili 5.4 wengi kati ya vifo hivyo vilikuwa si vya kawaida, kisheria na sio halali.
Amesema mikoa ambayo idadi hiyo imepatikana ni Dar es Salaam vifo 182, Mwanza 90, Mbeya 80 na Arusha 53.
Jaji Chande amesema kati ya vifo 518 watoto ni 21 ambapo 15 ni kati ya umri wa miaka 15-17 huku vifo vinne ni umri kati ya miaka saba na 10 na vifo viwili ni chini ya miaka mitano.
Pia, amesema vifo 205 vilikuwa ni vya raia sawa na asilimia 96.7 huku 16 sawa na asilimia 3.1 vilikuwa ni maofisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama.
“Kati ya watu 518 waliofariki dunia 373 walifikishwa hospitali wakiwa wamefariki na majeruhi 121 walifariki dunia wakati wanapata matibabu kwenye hospitali huku maiti 24 zilibainika hazina taarifa kamili,” amesema Jaji Chande.
Jaji Chande amesema kati ya maiti hizo 480 sawa na asilimia 92.7 zilitambuliwa na kuchukuliwa na familia zao.
Amesema chini ya uchunguzi wa vifo wenye mashaka katika hospitali mbalimbali za Rufaa Dar es Salaam na mikoani, maiti 260 zilifanyiwa uchunguzi na nyingine hazikufanyiwa kwa kukosekana kwa ridhaa za ndugu na familia.
“Maiti hizo hazikufanyiwa uchunguzi kwa kukosekana kwa ridhaa ya ndugu na familia ambazo zilitaka maiti za ndugu zao haraka ili wakazike,” amesema.
Amesema katika maiti hizo zilizofanyiwa uchunguzi nyingi zilibainika kuwa na majeraha ya kutobolewa na vitu vyenye ncha kali na kuvunjika katika sehemu mbalimbali za mwili.
Jaji Chande amesema majeraha hayo yalisababisha kupoteza damu nyingi hivyo kusababisha vifo hivyo, maiti 21 hazikuonyesha aina yoyote ya majeraha na maiti sita yalikuwa na majeraha ya moto.
Amesema maiti ambazo hazikuchukuliwa na ndugu 485 kati ya 518 zilitambuliwa na kuchukuliwa na ndugu zao kutoka vituo vya afya kwa ajili ya mazishi, lakini maiti sita pekee ambazo hazikutambuliwa na hazikuchukuliwa.
“Kati ya maiti hizo sita, imezikwa kwa mujibu wa kanuni za utupaji wa taka na mabaki ya miili ya binadamu na mamlaka za Serikali za mitaa ambao ndiyo utaratibu wa sheria nchini,” amesema.
Amesema hadi sasa kuna maiti tatu ambazo zipo Hopsitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam na tayari zimefanyiwa uchambuzi wa vinasaba (DNA).
Mbali na hivyo, amesema uchunguzi wa vinasaba ulifanyika kwenye maiti 274 kwa lengo la kuchukua taarifa za kutambua maiti kwa usahihi na taarifa hizo za kiuchunguzi zimesaidia kuwapa ndugu wa marehemu kwa ushahidi pale utakapohitajika.
“Tume ilifanya tathimini ya uchunguzi ulifanyika awali na madaktari waliothibitisha kifo kwenye hospitali mbalimbali kwa hiyo tume ilimwagiza mtaalamu na daktari bingwa wa pathelojia kufanya uchambuzi wa maiti ili kubaini sababu halisi na namna vifo hivyo vilivyotokea na maeneo ya mwili yaliyoathiriwa,” amesema.
Katika kutekeleza agizo hilo takribani maiti 219 zilifanyiwa uchambuzi wa kina na ulibainisha zilitokana na vifo visivyo vya kawaida. Ilibainika vifo 147 vilikuwa vya kuvuja damu nyingi, kujeruhiwa ubongo, kukosa hewa, kujeruhiwa uti wa mgongo, majeraha mbalimbali, mshtuko wa moyo na kifo kimoja sababu hazikujulikana.
Akieleza sababu halisi ya vifo, amesema vifo vingi katika idadi hiyo vilitokana na kupigwa risasi ambavyo ni vifo 197, sawa na asilimia 90 na vifo 22 sawa na asilimia 10 havikuhusiana na matumizi ya silaha za moto.
Taarifa za uchambuzi za wataalamu zimebainisha maiti 196 zilikuwa na majeraha sehemu za mkono na miguu na maiti 36 zilikuwa na majeraha sehemu ya kifua na tumbo na maiti 12 zilikuwa na majeraha sehemu za kichwa na shingo huku moja ikiwa haina baadhi ya viungo.