Vita vilivyoanzishwa na Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran vimekuwa na matokeo muhimu katika eneo la Asia Magharibi na hasa Ghuba ya Uajemi. Moja ya matokeo muhimu ya vita hivyo ni kuthibitika kwamba Marekani si mshirika wa kutegemewa na nchi za Kiarabu za eneo hilo.
Suali linaloulizwa ni, kwa sababu gani na ni kutokana na mwenendo na hatua gani, Marekani imethibitisha kuwa si mshirika wa kutegemewa na nchi za Kiarabu?
Sababu ya kwanza ya kuzifanya nchi za Kiarabu zipoteze imani kwa Marekani ni kutokana na namna nchi hiyo inavyoling’ang’ania na kulishupalia suala la kuuhami na kuulinda utawala wa kizayuni; na si vinginevyo. Marekani imethibitisha kuwa, kipaumbele chake cha kwanza katika sera ya Mashariki ya Kati ni kuhakikisha usalama na kudhamini maslahi ya Israel.
Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza hivi majuzi kuwa haijalishi kama watu wanaichukia Israel au la, muhimu ni kwamba Israel ni muitifaki wa Marekani. Katika vita vilivyoanzishwa dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, nchi za Kiarabu nazo pia zilipata madhara na hasara kubwa, lakini kipaumbele cha Washington kimekuwa ni kulinda na kudhamini maslahi ya Tel Aviv.
Sababu ya pili ya kuzifanya nchi za Kiarabu zipoteze imani kwa Marekani ni kuwa, kinyume na ilivyodaiwa, vituo vya kijeshi vya Marekani vilivyowekwa katika nchi hizo havijayahakikishia usalama mataifa hayo ya Kiarabu, bali vimehatarisha amani na usalama wao. Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ilieleza bayana wakati wa vita vya hivi karibuni, kwamba inaheshimu umoja wa ardhi za nchi za Kiarabu, lakini Marekani inazitumia ardhi hizo kufanyia mashambulio dhidi ya Iran. Kwa sababu hiyo, wachambuzi wengi wameeleza kuwa upo uwezekano wa nchi hizo za Kiarabu kufikiria upya suala la kuuweka rehani usalama wao kwa Marekani.

Sababu ya tatu inahusiana na yaliyojiri wakati wa urais wa Joe Biden nchini Marekani. Wakati Biden alipoingia madarakani, alizidisha mashinikizo na ukosoaji kwa Saudi Arabia katika suala la haki za binadamu na hata akamweka kwenye mtanziko mkubwa wa kisiasa kwenye uga wa kimataifa Mohammed bin Salman, mrithi wa ufalme wa nchi hiyo. Lakini moto wa mtazamo huo wa serikali ya Biden kuhusiana Saudia na Bin Salman ulikuja kupoa pale tu Marekani ilipojiona ina uhitaji wa mafuta ya Saudia kwa sababu ya vita vya Ukraine. Tukio hilo nalo pia lilionyesha kuwa, nchi za Kiarabu si washirika halisi wa Marekani na kwamba Washington inazichukulia kama nyenzo tu za kuzitumia kimaslahi nchi hizo.
Vita vya Ghaza pia vilizidisha hali ya kuzifanya nchi za Kiarabu zisiwe na imani na Marekani, kwa sababu, kwa upande mmoja, Washington iliunga mkono kwa hali na mali na kwa nguvu zote jinai za Wazayuni dhidi ya watu wa Ghaza, na kwa upande mwingine, Donald Trump alifika hadi hata kupendekeza ardhi za baadhi ya nchi za Kiarabu zitumike kwa ajili ya kuwapatia makazi Wapalestina na kuunda nchi yao ya Palestina.
Lakini nukta ya hitimisho ni kwamba, upotezaji imani unaoongezeka wa nchi za Kiarabu kwa Marekani unaweza kuwa sababu ya kuzifanya nchi hizo ziamue kustawisha zaidi uhusiano wao na madola hasimu na washindani wa Marekani, hususan China, na kulitumia suala la kuwa na uhusiano wa kimkakati na nchi hiyo na Russia kama ishara ya kujitegemea na kuwa huru kimaamuzi, sambamba na kujivua na utegemezi zilionao kwa Washington…/