
Dar es Salaam. Benki ya Stanbic Tanzania imezindua kampeni ya upandaji miti ijulikanayo kama Blue Roots, ikiwa na lengo la kupanda miti 50,000 nchini kama sehemu ya mkakati mpana wa kupanda miti milioni moja barani Afrika.
Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika Aprili 22, 2026 jijini Dar es Salaam, sambamba na maadhimisho ya Siku ya Dunia, ambapo viongozi na wafanyakazi wa benki hiyo walishiriki zoezi la upandaji miti wakionesha dhamira ya taasisi hiyo katika kulinda mazingira.
Mpango huo ni sehemu ya juhudi za kampuni mama ya benki hiyo, Standard Bank, unaolenga kuhamasisha sekta binafsi na jamii kushiriki kikamilifu katika uhifadhi wa mazingira huku wakichochea ukuaji wa uchumi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkuu wa Wateja Binafsi na Wateja Maalum wa Stanbic, Omari Mtiga, amesema kwa zaidi ya miaka 30 benki hiyo imekuwa mshirika wa maendeleo ya Tanzania kupitia kusaidia biashara na kukuza uchumi.
“Kupitia kampeni ya Blue Roots, tunaendeleza dhamira yetu ya kukuza uchumi huku tukilinda mazingira na kuacha thamani ya kudumu kwa vizazi vijavyo,” amesema Mtiga.
Kwa upande wake, Meneja Uendelevu wa benki hiyo, Annette Nkini, amesema upandaji miti ni uwekezaji muhimu katika mustakabali wa jamii na mazingira.
“Tunataka kuona matokeo chanya yanayogusa maisha ya watu na mazingira kwa vitendo kupitia programu hizi,” amesema Nkini.
Kwa mujibu wa benki hiyo, katika kipindi cha miaka mitano iliyopita tayari imepanda miti 102,850 nchini ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuboresha mazingira na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa uhifadhi wa mazingira.
Imeelezwa kuwa upandaji miti huchangia kuboresha ubora wa hewa, kulinda rutuba ya udongo na kuhifadhi vyanzo vya maji, hali inayosaidia kujenga mazingira bora ya kuishi.
Kupitia kampeni ya Blue Roots, Stanbic imeeleza kuwa itaendelea kushirikisha wafanyakazi, wateja na jamii kwa ujumla katika juhudi hizo, huku ikiitaka sekta binafsi na wananchi kuungana katika kulinda mazingira kwa maendeleo endelevu ya taifa.
Mbali na hilo, benki hiyo imeendelea kuwekeza katika sekta za elimu, afya, mazingira na elimu ya kifedha kupitia programu zake za uwajibikaji kwa jamii, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kukuza maendeleo shirikishi nchini.