Barcelona, Hispania. Ikiwa zimebaki 50 kuelekea katika michuano ya Kombe la Dunia itakayofanyika Marekani, Canada na Mexico, nyota wa Barcelona na timu ya taifa ya Hispania, Lamine Yamal huenda akashindwa kushiriki michuano hayo  baada ya kupata majeraha yaliyosababisha atolewe Uwanjani huku akimwaga machozi katika mechi ya Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’.

Winga huyo mwenye umri wa miaka 18, aliipa timu yake uongozi katika mechi dhidi ya Celta Vigo kwenye dimba la Camp Nou.

Yamal alifunga kwa mkwaju wa penalti aliousababisha yeye mwenyewe dakika ya 40 baada ya kuchezewa rafu.

 Hata hivyo, mara tu baada ya mpira kuingia wavuni, ilionekana alikuwa katika maumivu makali, yanayodaiwa kusababishwa na rafu aliyochezewa  au namna alivyoupiga mpira.

Lamine, hakushangilia bao hilo, badala yake alianza kutembea polepole huku akiwapa ishara madaktari kuna tatizo.

Alionekana kushika msuli wa nyuma wa paja la kushoto (hamstring) kabla ya kuanguka chini, akizungukwa na wachezaji wenzake waliokuwa wanakuja kumpongeza.

Nyota huyo aliufunika uso wake kwa mkono huku kocha wa Barcelona Hansi Flick akionekana kuwa na wasiwasi.

Baada ya kupatiwa matibabu kwa muda mrefu, alitolewa nje dakika ya pili ya muda wa nyongeza, akisaidiwa na madaktari huku akionekana kulia.

Flick alimfariji na kumkumbatia mchezaji wake nyota alipokuwa anatoka uwanjani kwa kuchechemea.

Majeraha hayo ambayo ukubwa wake utathibitishwa baada ya vipimo  yanaweza kuwa pigo kubwa kwa ndoto za Yamal kucheza Kombe la Dunia.

 Chipukizi huyo alikuwa ni miongoni mwa wachezaji  muhimu wakati Hispania iliposhinda taji la  Euro 2024, na alitarajiwa kuwa mhimili wa kikosi chao katika Kombe la Dunia.

Mashabiki walimiminika mitandaoni kumtia moyo, wakimuombea apone haraka ili arejee Uwanjani.

Penalti ya Yamal ndiyo iliyokuwa imezaa a bao pekee la mchezo huo ambao ulimalizika kwa Barca kushinda bao 1-0.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *