KOCHA wa Yanga Princess, Edna Lema amesema ameshtushwa na uamuzi wa kupewa kadi nyekundu katika mechi ya Ligi Kuu ya Wanawake dhidi ya Alliance Girls uliochezwa Uwanja wa Nyamagana.
Katika mechi hiyo ambayo Yanga ilishinda mabao 3-0, Lema alipewa kadi hiyo katika tukio ambalo alionekana akimgusa mwamuzi wakati akitoa maelezo ya kilichotokea uwanjani.
Akizungumza na Mwanaspoti, Lema amesema kuwa alichokuwa akifanya ni kutoa ufafanuzi kwa waamuzi kuhusu tukio lililotokea uwanjani, lakini hali ilibadilika ghafla na kusababisha kupewa adhabu hiyo.
“Tulikuwa tunaeleweshana tu na mwamuzi, sasa anadai nimemsukuma. Siwezi kuzungumzia hilo sana kwa sababu tayari limeshatokea,” amesema Lema.
Kwa mujibu wa video ya tukio hilo, Lema ambaye awali alikuwa amepewa kadi ya njano, alionekana akimweleza mwamuzi msaidizi namna mchezaji wake alivyosukumwa katika tukio la awali na wakati akijaribu kufafanua, alionekana kumgusa mwamuzi huyo kwa bahati mbaya kama sehemu ya maelezo yake.
Hata hivyo, mwamuzi msaidizi alionekana kukasirika ghafla na kumjibu kwa kumsukuma kwa nguvu katika eneo la shingo, ndipo mwamuzi wa kati aliitwa na kuelezwa tukio hilo, lakini bila uchunguzi wa kina alichukua uamuzi wa haraka wa kumpa kocha huyo kadi nyekundu.
Kadi hiyo inamfanya kocha huyo kukosa mechi tatu dhidi ya Geita Queens, vinara Simba (Mei 15) na Ceasiaa Queens (Mei 19).
Kifungu cha 41:5 ya kanuni ya ligi inaeleza kocha atakayekutwa na hatia ya kumshambulia kwa maneno mwamuzi, mchezaji au kiongozi kabla, wakati na baada ya mchezo atatapata adhabu za kusimamishwa mechi tatu na faini ya Sh500,000.
Adhabu hizo hazitahusu zinazotolewa na mwamuzi uwanjani.