Dar es Salaam. Ofisi ya Waziri Mkuu-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) amewataka maofisa lishe nchini kuongeza nguvu katika kukabiliana na changamoto za lishe kwani hali ya lishe nchini bado si ya kuridhisha.

Kati ya watoto 10, wenye umri chini ya miaka mitano, watatu kati yao wana udumavu na asilimia 58 ya watoto hao wanakabiliwa na upungufu wa damu.  

Hayo yamesemwa hivi karibuni jijini Dodoma na Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu-Tamisemi, Dk Jafar Seif wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Uratibu wa Huduma za Lishe kwa Maofisa Lishe kutoka Halmashauri zote 184 na mikoa 26 ya Tanzania bara.

Dk Seif amesisitiza hatua za haraka zinahitajika kubadili mwenendo wa viashiria hivyo, huku akiwataka wataalamu hao kuongeza uwajibikaji katika utekelezaji wa afua za lishe.

“Tatizo la upungufu wa damu limeathiri asilimia 56 ya wanawake wajawazito na asilimia 42 ya wanawake wenye umri wa kuzaa (kati ya miaka 15 – 49).

Aidha, asilimia 36 ya wanawake wenye umri wa miaka 20 – 49 wana uzito uliozidi, wanaume wenye umri wa miaka 20 – 49 wenye uzito uliozidi ni asilimia 17 hali hii inachochea kuongezeka kwa magonjwa sugu yasiyoambukizwa kama kisukari, shinikizo la damu na magonjwa ya moyo,” amesema. 

Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuwawezesha wataalam hao kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi ikiwa ni pamoja na kuongeza uwekezaji katika sekta ya lishe ambapo bajeti imeongezeka kutoka shilingi Bilioni 2 mwaka 2017/18 hadi kufikia bilioni 20.3 mwaka 2025/26.

Dk Seif amesema Serikali imeongeza nguvu kazi kwa kuajili  maofisa lishe 654 waliopangiwa vituo vya kazi katika mikoa na mamlaka za Serikali za mitaa kote nchini.

Vilevile Naibu Waziri alisisitiza umuhimu wa ubora wa takwimu, kuimarisha mpango wa chakula shuleni na kusimamia utekelezaji wa kanuni ya uongezaji wa virutubishikwenye vyakula ili kupunguza athari za matatizo ya lishe duninchini.

Kadhalika amewaelekeza maofisa hao, kuhakikisha wanasimamia ipasavyo matumizi ya rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya lishe, pamoja na kuimarisha utoaji wa elimu kwa jamii ili kuongeza uelewa wa wananchi kuhusu lishe bora na madhara ya utapiamlo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *