Dar es Salaam. Mamlaka nchini Marekani zinaamini kuwa mtu aliyekuwa amejihami kwa bastola Jumamosi iliyopita na kujaribu kuvamia hafla ya White House Correspondent’s Dinner katika hoteli ya Washington Hilton alimlenga Rais Donald Trump pamoja na maofisa wa serikali yake.                                                                                    

Hili linakuwa jaribio la tatu la kumuua Trump ndani ya kipindi cha chini ya miaka miwili, huku akiwa shabaha kuu ya mshambuliaji.                                

Matukio ya awali yalitokea mwaka 2024 katika jimbo la Pennsylvania na baadaye Florida.  

                                                                                

Kaimu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Todd Blanche, amesema amethibitisha hilo katika mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari nchini Marekani, na kuongeza kuwa mshukiwa huyo alisafiri kutoka California kwenda Washington kwa kutumia usafiri wa treni.

Maofisa wa usalama wamemtambua kwa jina la Cole Tomas Allen (31), ambaye alifyatua risasi karibu na ukumbi ambao Trump na wanahabari hao walikuwa wanakutana.

Trump na Makamu wake, JD Vance, pamoja na maofisa wengine wa serikali, waliondolewa haraka katika eneo hilo, huku mshukiwa huyo akikamatwa na anatarajiwa kufikishwa mahakamani leo, Jumatatu.

Maofisa wa usalama wakiimarisha ulinzi wakati jaribio linalodaiwa kuwa la kuumua Rais wa Marekan, Donald Trump. Picha na Mtandao

Trump aliliambia Shirika la Habari la Fox News kuwa uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mshukiwa huyo alikutwa na maandishi yanayoonesha kuwa anawachukia Wakristo.

Aidha, imebainika kuwa mshukiwa aliwasili Washington kwa kutumia treni, hali iliyomwezesha kusafirisha silaha bila ukaguzi mkali wa viwanja vya ndege. Pia, alikuwa mgeni katika hoteli hiyo, jambo lililompa nafasi ya kuwa ndani ya eneo la tukio kabla ya uchunguzi mkali kufanyika.

Maswali yaibuka

Shambulio hilo la risasi limeibua mjadala mzito kuhusu uimara wa mifumo ya usalama katika matukio makubwa yanayohusisha viongozi wa juu wa serikali ya Marekani.

Mshukiwa wa tukio hilo alifanikiwa kuvuka eneo la ukaguzi wa awali na kusogea karibu na sehemu iliyokuwa na Rais Trump pamoja na maofisa wengine waandamizi.

Uchunguzi wa awali unaonesha kuwa huenda alikuwa na nia ya kushambulia viongozi wa serikali, baada ya maandishi yake kupatikana yakionesha msimamo mkali dhidi ya Trump.

Pamoja na tukio hilo kuzua taharuki, Blanche amesema hatua zilizochukuliwa na walinzi zilikuwa za mafanikio makubwa. “Ni hadithi ya mafanikio ya kiusalama,” amesema alipozungumza na waandishi wa habari, akisisitiza kuwa maofisa walitekeleza wajibu wao ipasavyo.

Mashuhuda na wachambuzi wa masuala ya usalama wamesema walinzi wa United States Secret Service walichukua hatua za haraka kumkinga Rais Trump, wakimfunika na kumtoa jukwaani, huku maofisa wengine wakichukua nafasi za kimkakati kuzuia mshambuliaji kusogea zaidi.

Hata hivyo, video za tukio hilo zimezua maswali baada ya kumuonesha mshukiwa akikimbia karibu na eneo la ukaguzi bila kuzuiwa mapema. Baadhi ya wachambuzi wamesema hatua hiyo inaashiria uwezekano wa upungufu katika safu ya kwanza ya ulinzi.

Mtaalamu wa usalama na aliyewahi kuwa wakala wa Secret Service, Jonathan Wackrow, amesema si rahisi kufikia mazingira yasiyo na hatari kabisa. “Huwezi kuwa na usalama wa asilimia sifuri ya hatari, lakini kuna mambo ya kujifunza,” amesema.

Tukio hilo pia limeibua mjadala kuhusu uwepo wa viongozi wengi wakuu katika eneo moja. Ripoti zinaonesha kuwa Rais Trump na makamu wake walikuwepo katika hafla hiyo, jambo ambalo baadhi ya maofisa wa usalama hulichukulia kama hatari kubwa endapo kungetokea shambulio kubwa zaidi.

Kwa mujibu wa wachambuzi, uwepo wa viongozi wote wakuu katika hafla moja unaweza kuhatarisha mnyororo wa uongozi wa taifa iwapo tukio lingekuwa kubwa zaidi.

Katika uchambuzi wake, mwandishi wa CNN, Stephen Collinson, amesema tukio hilo linaakisi kuongezeka kwa vitendo vya vurugu vinavyohusiana na siasa nchini Marekani.

Amesema mashambulizi ya watu binafsi wenye misimamo mikali yanaendelea kutishia misingi ya demokrasia, ikiwemo uhuru wa kujieleza na mikusanyiko ya umma.

Pamoja na taharuki hiyo, Rais Trump amesisitiza kuwa hafla hiyo inapaswa kuendelea na hata kupangwa upya ndani ya muda mfupi. Amesema vitendo vya vurugu visipewe nafasi ya kushinda.

Wakati uchunguzi ukiendelea, mjadala mkubwa sasa ni iwapo hafla hiyo iendelee kufanyika kwa mfumo wa sasa au ibadilishwe, ikiwemo uwezekano wa kuitambua kama tukio la usalama wa kitaifa ili kuimarisha ulinzi zaidi.

Kwa ujumla, tukio hilo limeacha maswali mengi kuhusu usalama wa viongozi na mustakabali wa mikusanyiko mikubwa ya kisiasa, huku likionyesha changamoto zinazokabili demokrasia katika zama za sasa za ongezeko la vitendo vya vurugu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *