UNAPOFIKA Pemba kuna mambo mengi. Yapo mandhari na hadithi zake. Lakini, katika michezo kuna mchezo maarufu mchezo wa ng’ombe ambao zamani ulichezwa zaidi katika kipindi cha mavuno na umekuwa sehemu ya mila ya pekee kwenye kisiwa hicho.

Utamadani huo umetambulisha maeneo kadhaa ikiwemo Kijiji cha Pujini katika Mkoa wa Kusini Pemba na Mchangamdogo kwa ule wa Kaskazini.

Zamani mchezo huo ulichezwa sana na wanaume baada ya mavuno ikiwa ni sehemu ya sherehe za kumalizia shughuli hiyo salama, lakini jambo zuri bado unaendelezwa na vijana ingawa wanasema hawanufaiki kama enzi za mababu zao. Mchezo wa ng’ombe ni desturi inayojulikana hasa katika nchi za Hispania, Ureno na maeneo jirani ya Ufaransa eneo la Kusini, na katika koloni za zamani za Hispania huko Amerika kama Meksiko.

Mwanaspoti lilipata nafasi ya kukutana na katibu wa kikundi cha mchezo huo Pujini, Khamis Juma Hemed anayeelezea namna mchezo huo walivyourithi kutoka kwa wazazi.

Katibu huyo anasema sio kila ng’ombe anastahili kucheza mchezo huo, badala yake kuna sifa ambazo anapaswa kuwa nazo kwa lengo la kuunogesha na kwamba wao walirithi mchezo huo kutoka kwa wazazi wao kwa sababu ukitoa baada ya mavuno ilikuwa unachezwa kila Jumapili, hivyo nao wakavutiwa kujifunza na kuuendeleza utamaduni huo.

UNAVYOCHEZWA

Khamis anasema mchezo huo unachezwa kwenye uwanja mkubwa ulio safi ambao hujengwa kile kinachoitwa madungu yaani majukwaa kwa ajili ya watazamaji na chini kwa wachezaji, ambapo watazamaji hukaa juu ya madungu kuangalia huku mchezo ukichezwa chini na kwa maana hiyo hata mchezaji anapomshinda ng’ombe hawezi kuleta madhara kwa watazamaji.

Chini ya madungu hayo hujengwa jengo ambalo linaitwa bingili (yaani kibanda anachotumia mpiga zumari) ambacho kwa kawaida hukaliwa na wapiga zumari wa ng’ombe kwani huwa haingizwi moja kwa moja uwanjani isipokuwa hufungwa pembeni ya jengo hilo.

Baada ya kupigiwa zumari anatoka pembezoni mwa bingili na kufika uwanjani, na mchezaji huanza kucheza naye kwa uangalifu mkubwa.

“Mchezaji anatakiwa kuwa na khanga au kitenge hapo ndipo huanza kumuita (ng’ombe), na ukifanya hivyo anakufuata kisha unazunguka na kukimbia sehemu nyingine,” anasema Khamis.

Anasema wanatumia zumari kwa mchezo kumpigia ng’ombe masikioni mwake na maana yake ni kwamba huitumia kuamsha hasira na ukali wake. Katika mchezo huo watazamaji wanakuwa juu na wachezaji chini ya uwanja wanafanya hivyo huku wakizingatia usalama wa wananchi wanaofika eneo hilo.

SHERIA NA SIFA ZA MCHEZAJI, NG’OMBE

Khamis anasema ng’ombe anapoingizwa uwanjani sio kila mtu anaingia, isipokuwa mchezaji pekee anaruhusiwa kwani ndiye anayejua atumie mbinu za aina gani za kumgeuka ng’ombe huyo wanaposhindana.

Anasema ikitokea wameingia watu ambao hawahusiki na kila mmoja akawa anamuita mnyama huyo kwa wakati wake, hapo anaweza kuleta madhara kwa wengine. Hivyo, ndani ya uwanja anayeingia ni mchezaji mwenye uwezo wa kumuita na kucheza naye kwa namna anayoijua.

Akisimulia zaidi, anasema zipo sifa za mchezaji na ng’ombe husika, ambapo kwa mchezaji ni lazima ajifunze kwa lengo la kuzingatia namna ya kumgeuka ng’ombe wawapo uwanjani kwa sababu asipozingatia hilo anaweza kujikuta anajeruhiwa.

Inaelezwa kwamba mchezaji akishakumuita mnyama huyo wakati anapomfuata, ng’ombe humuangalia ili kutambua atumie njia ya kumgeuka kwa kupita na mchezaji hugeukia na kukimbilia sehemu nyingine. Ng’ombe wa mchezo huo anatakiwa kuwa ‘mpigaji’ kwa kuzingatia uwezo wake. Mfano, kabla ya kuingizwa kwenye mchezo huo anatazamwa uelekeo wa uwezo wa kumpiga mtu.

Khamis anasema ikiwa ng’ombe hana uwezo wa kumpiga mtu hawezi kufaa kwa ajili ya mchezo huo kwani wa aina hiyo hata mtoto anaweza kumshika bila ya athari na kwamba ng’ombe wa kucheza naye hatakiwi kuwa karibu na watu, hivyo anatafutiwa sehemu yenye pori (msitu) kwa ajili ya kuchungia huko.

Anafafanua kwamba ikiwa ng’ombe huyo atakuwa anawaona watu mara kwa mara atawazoea, hivyo ili kuepusha hilo ndio maana hufungwa msituni na akitoka huko ni kwa ajili ya shughuli ya uchezaji pekee na si vinginevyo.

Katibu huyo anasema mchezo huo unachezwa kwa kutumia nguo zenye rangi nyeupe kwa sababu huwa zinamvutia zaidi ng’ombe na inakuwa rahisi kumuona na kumfuata na kuwa, jamii ya Pemba imeukubali mchezo huo kwa sababu unapochezwa wananchi wanatoka maeneo mbalimbali ya Pemba kwenda kuburudika.

Kwa mchezo huo, sio tu wananchi hadi watalii wanaopata fursa kutembelea Pemba hufika kuangalia. Ng’ombe wa mchezo huo kuna wakati hukodishwa kwa hadi Sh100,000.

CHANGAMOTO SASA

Khamis anasema kwa sasa mchezo huo umekuwa ukipoteza uhalisia na ladha, kwani unachezwa kwenye matamasha maalumu ambako mara nyingi huwa mwaka hadi mwaka, jambo ambalo sio utamaduni ulivyo.

Anasema kwenye matamasha anachaguliwa mshindi kuanzia wa kwanza hadi wa tatu, lakini zawadi zinazotolewa hazikidhi mahitaji.

Pia, anasema wanapocheza wakati mwingine huumia, lakini baada ya tamasha hakuna msaada ambao wanaupata kutoka kwa waratibu.

Anasema katika tamasha moja walicheza kisha mwenzao mmoja aliumia baada ya kushindwa kumgeuka ng’ombe uwanjani na mchezo ulipomalizika alipatiwa Sh15,000 kwa ajili ya matibabu na kwa kuwa ilikuwa ndogo aliwarejeshea wahusika na na kujitibia kwa gharama zake.

OMBI KWA SERIKALI

Khamis anaiomba Serikali mchezo huo ubaki mikononi mwao ili uchezwe kama ilivyokuwa zamani na kwamba, awali mchezo huo ulikuwa unachezwa kila Jumapili na watazamaji walitozwa Sh1,000 kwa ajili ya kuangalia, jambo ambalo liliwafanya kuingiza kipato kupitia viingilio.

Anasema wanatamani mchezo huo ufike mbali zaidi kwani Tanzania mchezo huo upo kisiwani humo pekee na sehemu maarufu ni Pujini, ambako kikundi chao kina wachezaji wanane, hivyo wanachotaka ni kupewa uhuru wa kucheza popote nchini kwani matamasha yaliyopo hayawanufaishi.

Vilevile, anatoa wito kwa wachezaji wa ng’ombe na jamii kuwa na ushirikiano kwa lengo kuendeleza na kurithisha wengine mchezo huo.

CHUKUA HII

Mchezo huo ni sehemu ya kundi la michezo inayofanana na ule unaojulikana kama Mancala ambao umeenea katika nchi nyingi za Afrika, Asia na baadhi ya maeneo ya Mashariki ya Kati. Katika maeneo ya Pwani ya Afrika Mashariki kama Pemba uliendelezwa zaidi na kuwa sehemu ya utamaduni wa jamii ukitumika kama burudani na njia ya kujifunza mbinu, hesabu na fikra za kimkakati.

Mara nyingi ulikuwa unachezwa na watu wazima hasa wanaume, ingawa vijana pia walikuwa wakijifunza. Jina ‘mchezo wa ng’ombe’ linatokana na istilahi za ndani zinazotumika kuelezea mbegu au vipande vinavyochezewa, ambavyo hupewa majina ya kitamaduni kama ‘ng’ombe’ kuonyesha thamani au nguvu katika mchezo. Kwa kifupi, asili ya mchezo wa ng’ombe ni jadi ya Kiafrika ukiwa ni sehemu ya urithi wa utamaduni unaorithishwa kizazi hadi kizazi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *