Dar es Salaam. Kampuni ya mawasiliano ya Yas Tanzania imezindua rasmi kampeni yake mpya ijulikanayo kama ‘Zingatia Mtandao wa Viwango’, ikiwa ni sehemu ya mkakati wake wa kuendelea kuimarisha ubora wa huduma za mawasiliano na kuhakikisha Watanzania wanapata huduma za kidijitali zenye uhakika na viwango vinavyokubalika kimataifa.

Kupitia kampeni hiyo, kampuni inalenga kuhamasisha watumiaji wa huduma za mawasiliano nchini kuelewa na kuthamini umuhimu wa kutumia mtandao wenye ubora wa juu, unaowezesha mawasiliano ya uhakika, intaneti ya kasi pamoja na upatikanaji wa huduma za kidijitali bila vikwazo.

Uzinduzi wa kampeni hiyo unakuja sambamba na hatua kubwa ambazo kampuni hiyo imechukua katika uwekezaji wa miundombinu ya mawasiliano. Yas Tanzania imewekeza zaidi ya Sh1 trilioni katika upanuzi na uboreshaji wa mtandao wake, hatua inayoiweka miongoni mwa kampuni zilizo na mtandao mpana na unaofikia maeneo mengi zaidi nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa uzinduzi huo juzi, Afisa Mkuu wa Teknolojia na Ufundi wa kampuni hiyo, Emmanuel Mallya, alisema baada ya mafanikio ya kujenga mtandao imara, sasa lengo kuu ni kuhakikisha Watanzania wanapata manufaa halisi ya uwekezaji huo katika nyanja mbalimbali za maisha yao ya kila siku.

“Baada ya kujenga mtandao imara, sasa tunataka Watanzania wanufaike zaidi iwe ni kwenye shughuli za kiuchumi, elimu, burudani, kilimo au mawasiliano ya kila siku,” alisema Mallya.

Alieleza kuwa kampuni hiyo kwa sasa ina zaidi ya minara 4,800 ya mawasiliano, ikiwa ni idadi kubwa kuliko mtoa huduma mwingine yeyote nchini. Miundombinu hiyo imewezesha kufikiwa kwa zaidi ya asilimia 95 ya Watanzania katika maeneo ya mijini na vijijini, hatua inayochangia kupunguza pengo la kidijitali.

Mbali na kuongeza minara, Yas pia imewekeza kwa kiasi kikubwa katika miundombinu ya nyaya za mawasiliano ya kasi (faiba) pamoja na kuimarisha teknolojia ya mtandao wake kutoka 2G hadi 4G, huku ikiendelea kuanzisha huduma za 5G katika baadhi ya miji ya kimkakati nchini. Maboresho hayo yameongeza kasi ya intaneti, ubora wa mawasiliano na uthabiti wa huduma kwa wateja wake.

Kwa mujibu wa Mallya, ubora wa mtandao wa kampuni hiyo umetambuliwa pia katika ngazi ya kimataifa. Alisema kampuni ya Ookla, inayojulikana kwa vipimo vya kasi ya intaneti kupitia mfumo wa Speedtest, imeitambua Yas kuwa mtandao wenye kasi zaidi nchini kwa miaka mitatu mfululizo.

“Mtandao wa Viwango siyo kasi tu ni uwezo wa Watanzania kufanya zaidi kila siku, popote walipo. Leo, mteja wa Yas anaweza kufanya biashara mtandaoni kwa ufanisi, kujifunza bila vikwazo na kufurahia burudani bila kusuasua,” alisisitiza.

Aidha kupitia kampeni ya ‘Zingatia Mtandao wa Viwango’, Yas Tanzania inalenga kuweka msingi mpya wa matumizi ya mtandao nchini, ambapo huduma za mawasiliano hazitachukuliwa tena kama anasa, bali kama nyenzo muhimu ya kufungua fursa za kiuchumi, kijamii na kielimu kwa Watanzania wote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *