Timu za Kajuna ya Kigoma na Kahama Madini ya Shinyanga, zimekata tiketi ya kushiriki Ligi Daraja la Pili (First League) msimu ujao baada ya leo Alhamisi, Aprili 30, 2026, kuibuka na ushindi katika mechi zao za nusu fainali za mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Mikoa (RCL) zilizochezwa katika Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.

Kwa mujibu wa kanuni, timu mbili zinazoingia hatua ya fainali ya RCL zinafuzu moja kwa moja katika First League huku zinazoshika nafasi ya tatu na nne zikicheza mchujo kuwania nafasi nyingine mbili.

Kahama Madini ndio imekuwa ya kwanza kufuzu First League baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Stand Masasi katika mchezo wa kwanza ulioanza saa 8:00 mchana.

Kahama Madini imelazimika kutoka nyuma na kuibuka na ushindi katika mchezo huo baada ya kutanguliwa kufungwa bao na Stand Masasi.

Bao la Stand Masasi limepachikwa katika dakika ya 42 na Anuary Musa lakini mabao ya Masatu Charles katika dakika ya 60 na Aryan Mwaisenga katika dakika ya 84 yalitosha kupeleka furaha mkoani Shinyanga.

Katika mchezo wa pili, wenyeji Kajuna ya Kigoma wamemaliza kwa ushindi wa kishindo wa mabao 8-0 dhidi ya Mount Hanang ya Manyara.

Mabao ya Kajuna katika mchezo huo yamepachikwa na Amos Chisongela na Abeid Mbogo waliofunga mawili kila mmoja huku mengine yakiwekwa kimiani na John John, Ally Omary, Yusuph Kakoko na Abasi Amad.

Mechi ya fainali baina ya Kajuna FC na Kahama Madini imepangwa kuchezwa Jumamosi, Mei 2, 2026 kuanzia saa 9:30 alasiri.

Mechi hiyi itatanguliwa na mchezo wa kuwania mshindi wa tatu baina ya Mount Hanang na Stand Masasi itakayochezwa siku hiyohiyo kuanzia saa 7:00 mchana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *