HATIMAYE, Simba imevunja rekodi ya Yanga iliyodumu kwa siku 538 ya kutopoteza mechi katika mashindano ya ndani, baada ya timu hiyo kushinda bao 1-0 katika fainali ya Kombe la Muungano iliyopigwa Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Aprili 29, 2026.
Yanga iliingia na kumbukumbu nzuri baada ya kutwaa taji hilo mwaka 2025, baada ya kuifunga JKU bao 1-0, lililofungwa na Maxi Nzengeli, katika fainali iliyopigwa Uwanja wa Gombani kisiwani Pemba, Mei 1, 2025.
Hata hivyo, licha ya morali kubwa kwa Yanga, lakini ilijikuta ikipoteza dhidi ya Simba kwa kukubali kichapo cha bao 1-0, lililofungwa na Seleman Mwalimu ‘Gomez’, dakika ya 118 kwa penalti, baada ya dakika 90 kuisha suluhu (0-0).
Bao hilo la Seleman Mwalimu ‘Gomez’, alilifunga kwa umaridadi mzuri kwa mkwaju wa penalti uliosababishwa na kiungo wa Simba, Clatous Chota Chama ‘Triple C’, aliyechezewa madhambi akiwa eneo la hatari na winga wa Yanga, Edmund John.
Katika fainali hiyo ya Kombe la Muungano iliyopigwa kwenye Uwanja wa New Amaan, Complex visiwani Zanzibar, Simba ilitwaa taji hilo likiwa la saba kwa kikosi hicho na kuifikia rekodi ya Yanga, tangu mashindano hayo yalipoanza mwaka 1982.
Ubingwa huo ambao ni wa saba kwa Simba, ulikuwa pia ni wa pili kwa kikosi hicho, tangu michuano ya Kombe la Muungano iliporejea 2024, baada ya kushindwa kufanyika kwa kipindi cha miaka 22, tangu mara ya mwisho ilipofanyika mwaka 2002.
Ushindi huo wa Simba, umeifanya kuvunja rekodi ya Yanga ya kutopoteza mechi katika mashindano ya ndani, kwani timu hiyo tangu ilipochapwa mabao 3-1, dhidi ya Tabora United kwa sasa TRA United, kwenye Ligi Kuu Bara, ilikuwa haijapoteza tena.
Katika mechi hiyo ambayo ni ya msimu wa 2024-2025 iliyochezwa Novemba 7, 2024, kwenye Uwanja wa Azam Complex jijini, Dar es Salaam, ilikuwa ya mwisho kwa Yanga kupoteza, hadi Simba ilipovunja mwiko huo baada ya kudumu muda mrefu.
Tangu Novemba 7, 2024, Yanga ilikuwa imecheza jumla ya mechi 64 za mashindano yote ya ndani, kuanzia Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho la CRDB, Ngao ya Jamii, Kombe la Muungano na Kombe la Mapinduzi, bila ya kupoteza, hadi Simba ilipotibua rasmi rekodi hiyo.
Kiujumla, tangu Novemba 7, 2024, Yanga imecheza mechi 65 za mashindano hayo ya ndani, ambapo kati ya hizo, imeshinda 58, sare sita na kupoteza moja dhidi ya Simba, huku ikifunga jumla ya mabao 177 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 16.
Katika Ligi Kuu, timu hiyo imecheza mechi 39, ikishinda 33 na kutoka sare sita, ikifunga mabao 113 na kuruhusu tisa tu, huku kwenye Kombe la CRDB imecheza 15 na kushinda zote, huku kikosi hicho kikifunga jumla ya mabao 48 na kuruhusu manne.
Kwenye Ngao ya Jamii ambayo ni fainali ya mwaka 2025, Yanga ilishinda bao 1-0, dhidi ya Simba, huku Kombe la Muungano la 2025, iliyotwaa ubingwa, ilishinda mechi zote tatu na kushuhudia kikosi hicho kikifunga jumla ya mabao manne na kuruhusu moja.
Katika Kombe la Mapinduzi 2026, iliyotwaa pia ubingwa kwa kuifunga Azam FC kwa penalti 5-4, baada ya suluhu (0-0), Yanga ilicheza mechi nne hadi kufika fainali, ambapo kati ya hizo ilifunga jumla ya mabao matano bila kuruhusu nyavu zake kutikiswa.
Mwaka 2026 katika Kombe la Muungano, Yanga ilicheza mechi tatu ikianza kwa kuifunga Mwembe Makumbi City mabao 4-0 na kuifunga Azam FC 2-1, kisha kutinga fainali na kuchapwa bao 1-0 dhidi ya Simba na kutibuliwa rasmi rekodi yake.
Ushindi huo wa Simba, umeifanya kuvunja uteja kwa Yanga, kwa sababu kabla ya hapo mara ya mwisho timu hiyo kushinda pia ilikuwa ni katika fainali ya Ngao ya Jamii kwa penalti 3-1, baada ya suluhu (0-0), mechi iliyopigwa, Agosti 13, 2023.
Kwa maana hiyo, tangu mara ya mwisho Yanga ilipochapwa na TRA United mabao 3-1, Novemba 7, 2024, katika mashindano ya ndani, Simba imeivunja rekodi hiyo, iliyodumu kwa siku 538, ambazo ni sawa na mwaka mmoja, miezi mitano na siku 22.
Katika kipindi hicho cha siku 538, Yanga imekutana na Simba mara nne kwenye mashindano matatu tofauti. Yanga imeshinda mbili, imepoteza moja sawa na sare.
Matokeo ya mechi hizo yapo hivi; Yanga 2-0 Simba (Ligi Kuu, Juni 25, 2025), Yanga 1-0 Simba (Ngao ya Jamii, Septemba 16, 2025). Sare ni ya 0-0 katika Ligi Kuu Bara (Machi 1, 2026) na kipigo cha 1-0 katika Kombe la Muungano (Aprili 29, 2026).