Geita. Wafanyakazi kutoka idara tofauti mkoani Geita, wameiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kutenga fedha kwaajili ya vifurushi vya Intaneti, ili kuwawezeaha utumaji wa taarifa na madokezo kwa waajiri wao kwa wakati.

Kutokana na kupanda kwa gharama za maisha nchini na baadhi ya watumishi kuishi mazingira ya vijijini,wamekuwa wakitumia gharama kubwa kwenye kununua bando la Intaneti huku vipato vyao vikiwa havikidhi uhitaji wao.

Ombi hilo limetolewa leo ijumaa Mei mosi,2026,na Katibu wa Chama cha Walimu (CWT) Mkoa wa Geita,Pauline Tinda, wakati akisoma risala kwa niaba ya Shirikisho la vyama vya Wafanyakazi (Tucta) katika maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani kimkoa katika Uwanja wa Shule ya Msingi Ludete, Kata ya Ludete, mji mdogo wa Katoro wilayani Geita.

Katika taarifa yake,Tinda amesema mifumo ya utendaji kwa watumishi wa Serikali Pepmis, imekuwa na Changamoto wakati wa ujazaji wa taarifa na madokezo ya kiutendaji huku baadhi ya maeneo hasa ya vijijini,yakikabiliwa na mifumo duni ya intaneti.

“Watumishi huingia gharama kununua bando kwakuwa wanalazimika kuingia kwenye mifumo kila siku ili kujaza taarifa na madokezo mbalimbali. Pia, baadhi ya maeneo kukosa mtandao kunasababisha watumishi kushindwa kuwazilisha taarifa zao kwa wakati.”

Akijibu risala hiyo, Mkuu wa mkoa wa Geita, Martine Shigela amewaagiza wakurugenzi na maofisa utumishi mkoani humo, kutenga bajeti ya posho na motisha kwa wafanyakazi ili kuwarahisishia wafanyakazi utumaji wa taarifa kwenye mifumo kwa wakati huku Serikali ikiendelea kuboresha upatikanaji wa Intaneti maeneo ya vijijini.

“Serikali imajipanga vizuri mnamo mwezi wa nne ilizindua minara zaidi ya 700 katika maeneo yenye changamoto ya mtandao,lakini pia itaendelea kuboresha upatikanaji wa mtandao pamoja na nishati ili kila Wilaya ifikiwe na mkongo wa taifa wa mawasiliano,” amesema RC Shigela.

Pia Shigela amewataka waajiri mkoani humo kudumisha mazungumzo na wafanyakazi kupitia uchambuzi wa mara kwa mara, kuhusu taasisi zao ili kutatua kero zibazowakabili watumishi wao kupitia uwazi.

Katika hatua nyingine Shigela ametoa rai kwa wakurugenzi kutoa kipaumbele kwa watumishi wanaoomba vibali vya kwenda masomoni ili kuwapa motisha ya kufanya kazi zao kwa weledi kwa kuendana na mabadiliko ya Teknolojia.

Maadhimisho hayo yamebebwa na kaulimbiu isemayo “Kazi zenye staha ni nguzo imara kwa maendeleo endelevu katika utekelezaji wa Dira ya Taifa 2050”.

Kutokana na Dira ya taifa kuweka kipaumbele cha asilimia 70 kwa Sekta binafsi katika kufikia Maendeleo endelevu,mgodi wa GGML ambao ni moja ya wadau wa Maendeleo mkoani humo,wameahidi kuendelea kutoa kipaumbele cha ajira kwa wazawa sambamba na utoaji elimu ya usalama kwa wakazi wanaozunguka mgodi huo.

Akizungumza na Mwananchi, Ofisa utumishi kutoka Mgodi wa Geita Gold Mine (GGML), Ramadhan Burude amesema kupitia kaulimbiu hiyo inayohimiza utu wenye staha, wamekuwa wakitoa motisha na tuzo kwa watumishi wao ili kuongeza ushindani sambamba na kudumisha ushirikiano na wananchi.

“Tumekuwa tukitoa vifaa vya kisasa kwa wafanyakazi na elimu pindi anapoajiriwa na hata anapotoka likizo,lakini pia wananchi tumekuwa tukiwapatia elimu kuhusu usalama hasa maeneo yanayozunguka mgodi,” amesema

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *