
Iringa. Wananchi wa Wilaya ya Mufindi mkoani Iringa wameeleza matarajio yao makubwa kuelekea ziara ya Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba, anayetarajiwa kufanya ziara ya kikazi Mei 2 hadi 3, 2026 katika maeneo mbalimbali ya wilayani humo.
Wakizungumza na Mwananchi Digital leo Mei Mosi, 2026 Wananchi hao wamesema ziara hiyo imepokewa kwa matumaini makubwa kwao na ni fursa muhimu ya kuwasilisha changamoto zao moja kwa moja kwa kiongozi huyo wa juu serikalini.
Mkazi wa Kijiji cha Igowole, Moses Mwakalobo, amesema wananchi wanatarajia Waziri Mkuu atatoa mwelekeo wa kuboresha na miundombinu ya barabara hasa Mafinga – Mgololo Wilayani humo.
“Tunafurahi kumpokea Waziri Mkuu kwa sababu hii ni nafasi ya kueleza changamoto zetu, hasa kwenye barabara na upatikanaji wa dawa hospitalini,” amesema Mwakalobo.
Baadhi ya wananchi wa Mufindi Kaskazini wamesema ujio wa Waziri Mkuu ni fursa muhimu ya kuwasilisha madai yao ya muda mrefu kuhusu stahiki wanazodai kutoka katika kiwanda cha chai kilichopo eneo hilo, wakieleza kuwa wamekuwa wakisubiri kwa muda mrefu kupata haki zao bila mafanikio ya kuridhisha.
“Tunamkaribisha Waziri Mkuu kwa matumaini makubwa kwa sababu tunaamini sauti yetu itasikika, hasa kwenye suala la stahiki zetu ambazo zimekuwa zikitusumbua kwa muda mrefu.” amesema mmoja wa wananchi Mufindi ambaye jina lake hakutaka kujulikana
Kwa upande wake, Neema Mhando kutoka Mafinga amesema vijana wengi wanatarajia kusikia kauli ya Serikali kuhusu ajira na uwezeshaji wa kiuchumi.
“Vijana wa Mufindi tunahitaji mitaji na fursa za kiuchumi na ujio wa Waziri Mkuu unatupa matumaini ya kusikilizwa,” amesema Neema.
Kwa mujibu wa wananchi hao, mikutano ya hadhara itakayofanyika katika ziara hiyo itatoa nafasi kwa wananchi kueleza changamoto zinazowakabili na kupokea majibu ya moja kwa moja kutoka kwa Waziri Mkuu.
Wananchi wengine wameeleza kuwa ujio huo utaongeza uwajibikaji kwa viongozi wa ngazi za chini, hasa katika usimamizi wa miradi ya maendeleo inayoendelea ndani ya wilaya hiyo.
Aidha, wafanyabiashara wa Mafinga wameeleza matarajio yao ya kuona Serikali ikiendelea kuboresha mazingira ya biashara katika miundombinu na upatikanaji wa huduma za kifedha.
Wakulima wa Mufindi nao wamesema wanatarajia kusikia mikakati ya Serikali kuhusu pembejeo, masoko ya mazao, na bei ya mazao yao.
Kwa ujumla, wananchi wa Mufindi wameonyesha utayari mkubwa wa kushiriki kikamilifu katika ziara hiyo kwa matumaini ya kupata majawabu ya changamoto zao na kuona kasi mpya ya maendeleo katika maeneo yao.
Awali Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James akizungumza na wanahabari kuhusu ujio huo wa Waziri Nchemba, amesema ziara hiyo inalenga kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kusikiliza changamoto za wananchi ili kuwasilisha kero zao na kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa Serikali.