Vikosi vya jeshi la Mali vimedhibiti tena mji wa karibu na mpaka wa nchi hiyo na Niger baada ya wanamgambo wanaohusishwa na ISIS kuondoka katika eneo hilo kufuatia mapigano makali, wakati jeshi likiimarisha doria kwenye maeneo hayo.

Wakazi wa maeneo hayo wamesema vikosi vya jeshi la Mali vimedhibiti tena mji wa mpakani karibu na Niger baada ya wanamgambo wanaohusishwa na ISIS kuvamia mji huo mapema wiki hii.

Wakazi wawili wa mji wa Ménaka, karibu na mpaka wa Niger, wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba wapiganaji wa ISIS wameondoa katika eneo hilo kufuatia mapigano na jeshi, ambalo limeanza tena doria za nchi kavu na angani. Chanzo cha kidiplomasia pia kimethibitisha kuwa wanajeshi wa Mali wamechukua tena udhibiti wa eneo hilo.

Katika eneo la kati la Mopti, ambalo pia lilikumbwa na mashambulizi ya waasi mwishoni mwa wiki iliyopita, hali ya utulivu ilirejea kufikia Jumatano, ingawa wakazi wa mji huo wako katika hali ya tahadhari.

Kiongozi wa Mali, Assimi Goïta alionekana hadharani kwa mara ya kwanza Jumanne iliyopita tangu waasi na muungano wa makundi yanayotaka kujitenga kuanzisha mashambulizi yao Jumamosi iliyopita, ambayo yalipelekea kuuawa Waziri wa Ulinzi wa Mali, Sadio Camara.

Baada ya kutoweka hadharani kwa siku kadhaa, Goïta aliahidi kuwaangamiza wale waliohusika na mashambulizi ya Jumamosi, ambayo yalifanyika kwa ushirikiano wa wanamgambo na kundi la Azawad Liberation Front, ambao waliteka mji wa kimkakati wa Kidal.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *