Malalamiko yameendelea kumiminika baada ya Muisraeli mwenye misimamo mikali kumshambulia mtawa wa kike raia wa Kifaransa, huku Waisraeli Wazayuni wakishadidisha mashambulizi dhidi ya Waislamu na Wakristo pamoja na maeneo matakatifu katika ardhi za Palestina zinazokoloniwa na utawala wa Israel.

Askofu William Shomali, naibu wa Patriarka wa Kanisa Katoliki la Kilatini katika al-Quds (Jerusalem), amesema kuwa alitazama video ya tukio hilo la kusikitisha la hujuma dhidi ya mtawa huyo wa Kikristo na kulitaja kuwa “lenye uchungu, la kutisha, na zito sana.”

Ameongeza kuwa: “Mtawa huyo wa kike hivi sasa ni dhaifu kiafya. Mshambuliaji alimsukuma kwa nguvu kutoka nyuma, na kumsababisha aanguke chini baada ya kichwa chake kugonga jiwe lililoinuka. Kisha alirudi na kumkanyaga kabla ya kuzuiwa.”

Askofu Shomali pia amesisitiza “hitaji la kutoa elimu kwa wale wenye itikadi za kibaguzi.”

Ameongeza: “Mshambuliaji kurudi tena na kumpiga teke baada ya kumuumiza tayari kunafanya kitendo hiki kuwa cha ukatili mkubwa zaidi.”

Kuhusu kukamatwa kwa mshambuliaji huyo wa Kizayuni, amesema polisi wa utawala wa Israel “hawajakuwa wakichukua hatua za haraka katika matukio mengine kama haya.”

Aidha, Askofu Mkuu Ataullah Hanna, ambaye ni mkuu wa Kanisa la Othodoksi la Kigiriki katika mji wa al-Quds (Jerusalem), ameonya kuwa matukio ya aina hii “yanaakisi wasiwasi unaoongezeka kuhusu mustakabali wa uwepo wa Kikristo katika Ardhi Takatifu inayokaliwa kwa mabavu.”

Katika ujumbe wa mitandao ya kijamii, Askofu Hanna amesema kuwa “shambulio dhidi ya mtawa katika mji wa al-Quds linakuja katikati ya ukiukaji unaozidi dhidi ya taasisi za Kikristo mjini humo.”

Katika ujumbe huo, alionya kuwa mashambulizi kama haya “hayako tena katika sura ya matukio ya hapa na pale, bali ni muendelezo unaotishia uwepo wa Kikristo.”

Ameitaka pia jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua kukomesha ukatili huo.

Miaka ya karibuni imekuwa na ongezeko dhahiri la mashambulizi ya walowezi wa Kizayuni dhidi ya viongozi wa Kiislamu na Kikristo pamoja na maeneo matakatifu katika eneo la al-Quds Mashariki.

Shambulio hili linakuja baada ya video iliyosambaa mwezi uliopita, ikimuonyesha askari wa jeshi la Israel akibomoa sanamu ya Nabii Isa, ambayo ni nembo ya Ukristo, kwa nyundo kubwa—tukio ambalo limelaaniwa duniani kote.

Viongozi wa Kanisa wamekuwa wakitoa wito mara kwa mara kwa mamlaka za Israel kuchukua hatua thabiti kukomesha mashambulizi kama haya. Hata hivyo, wakuu wa Israel hawachukui hatua, jambo ambalo limepelekea matukio kama hayo kuongezeka.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *