BEKI wa kushoto wa Barberian FC, Hamza Shabani amesema licha ya mwenendo mbaya wa timu hiyo msimu huu hadi sasa katika Ligi ya Championship, bado hawajakata tamaa kwa sababu tofauti ya pointi na wapinzani wao waliokuwa juu siyo kubwa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Hamza amesema kinachotokea ni upepo mbaya wanaokutana nao, japo wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wanafanya kazi yao ipasavyo, hivyo watapambana hadi mwisho kwa mechi zote zilizobakia ili wasishuke daraja.
“Siwezi kusema mabadiliko ya mara kwa mara ya benchi la ufundi ndiyo yaliyotufikisha hapa tulipo leo, kinachotokea kwetu naona ni upepo mbaya tunaokutana nao, bado tuna nafasi ya kupambana, japo jitihada zaidi zinahitajika,” amesema Hamza.
Nyota huyo aliyeanzia kucheza Gwambina FC kuanzia ya vijana chini ya miaka 20 hadi ya wakubwa, amesema lengo kubwa kwa sasa ni kupambana ili kupata nafasi ya kucheza mechi za ‘Play-Off’ za kubakia katika ligi msimu ujao.
Barberian FC kabla ya mechi ya jana dhidi ya Gunners FC, imecheza 23, ikishinda moja, sare saba na kupoteza 15, imefunga mabao 12 na kuruhusu 36 na iko mkiani nafasi ya 16 na pointi 10.