DAR ES SALAAM: Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (TISEZA) kwa kushirikiana na TIB Development Bank wamesaini hati ya makubaliano (MoU) yenye lengo la kuimarisha uhamasishaji wa uwekezaji, kukuza uwezo wa biashara na kuharakisha maendeleo ya maeneo maalum ya kiuchumi nchini.
Kupitia makubaliano hayo yamefanyika leo Mei 5 jijini Dar es Salaam, taasisi hizo mbili zinatarajia kurahisisha upatikanaji wa mitaji kwa wawekezaji, hatua itakayochochea ukuaji wa viwanda, biashara na ajira katika maeneo maalum ya kiuchumi.
Akizungumza kuhusu ushirikiano huo, Mkurugenzi Mkuu wa TISEZA, Gilead Teri amesema makubaliano hayo ni hatua muhimu katika kuvutia uwekezaji na kuongeza tija ya shughuli za kiuchumi nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo Tanzania, Deogratius Kwiyukwa amesema benki hiyo itaendelea kushirikiana na TISEZA katika kuhakikisha wawekezaji wanapata huduma za kifedha kwa urahisi ili kufanikisha miradi yao.
Ushirikiano huo unatarajiwa kuongeza kasi ya maendeleo ya maeneo maalum ya kiuchumi pamoja na kuimarisha mchango wa sekta binafsi katika ukuaji wa uchumi wa taifa.