Dodoma. Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amemuomba mshambuliaji wa zamani wa timu ya Taifa ya Ivory Coast na Chelsea ya England, Didier Drogba kuwa Balozi wa Tanzania kuelekea Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027.

Michuano hiyo mikubwa barani Afrika ya mpira wa miguu itaandaliwa kwa pamoja na nchi za Tanzania, Uganda na Kenya.

Ombi hilo limetolewa leo Jumanne, Mei 5, 2026, wakati ambao Rais Samia amekutana na Drogba, Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.

Rais Samia Suluhu Hassan akisalimiana na Didier Drogba mara baada ya kuwasili Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Aidha, Rais Samia ameitaka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo kushirikiana na mchezaji huyo kubadilishana uzoefu wa kuendesha vituo vya michezo nchini (Sports Academy).

Mchezaji huyo amemshukuru Rais Samia na kuonesha utayari wa kushirikiana na Serikali.

Pamoja na mafanikio kadhaa aliyoyapata katika mpira wa miguu, mwaka 2005, alifanya ushawishi uliosaidia kusitishwa kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini kwao vilivyodumu kwa miaka kadhaa.

Rais Samia Suluhu Hassan akiwa kwenye picha ya pamoja na Didier Drogba, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.

Drogba ni miongoni mwa nyota wa soka wanaoheshimika ndani na nje ya bara la Afrika kutokana na kiwango bora alichoonyesha na mafanikio aliyoyapa wakati alipokuwa akicheza soka la ushindani.

Katika ngazi ya klabu, Drogba amewahi kunyakua zawadi ya Ufungaji Bora wa Ligi Kuu ya England mara mbili ambazo ni katika misimu ga 2006/2007 na 2009/2010 lakini pia amewahi kutwaa kiatu cha ufungaji bora wa Kombe la UEFA msimu wa 2003/2004 akiwa na Marseille ya Ufaransa.

Mchango wake kwa timu ulimfanya Drogba atwae mataji 14 akiwa na Chelsea aliyoitumikia kuanzia 2004 hadi 2012.

Mataji hayo 14, moja ni la Ligi ya Mabingwa Ulaya, matano ya Ligi Kuu England, manne ya FA, matatu ya Kombe la Ligi na Ngao ya Jamii mara mbili.

Pia alishinda mataji matatu tofauti akiwa na Galatasaray ya Uturuki.

Mafanikio makubwa ambayo aliyapata akiwa na jezi ya timu ya Taifa ya Ivory Coast ni kumaliza katika nafasi ya pili mara mbili kwenye Fainali za AFCON 2006 na 2012.

Mchezaji huyo ameichezea Ivory Coast idadi ya mechi 95 na kuifungia mabao 63.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *