Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan, amemtaka bosi mpya wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), Kheri Mahimbali kuisimamia vyema taasisi hiyo ili kiwe chombo cha Serikali chenye matumaini.

Leo Jumatano, Mei 6, 2026 Ikulu ya Dodoma, Samia amewaapisha viongozi aliowateua na kushuhudia wakila viapo vya maadili ambapo amesema kwa mujibu wa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kuna mambo hayajasimama Temesa na maswali mengi yasiyojibika.

“Temesa sasa unalipeleka gari wanalikagua, wanakwambia hili gari lina ubovu huu na huu, lakini sisi vifaa hatuna wala hatuna… wanakuandika ili upeleke nje kumbe kwenye gereji wanazozijua,” amesema.

“Au mafundi haohao wanakwambia sisi tuna uwezo wa kulitengeneza nunua hiki na hiki, tutalitengeneza.Ukiangalia ripoti ya CAG ya mwaka huu utaona mapungufu yaliyopo naomba ukayasimamie,” amesema Rais Samia.

Samia amemtaka Mahimbali kushirikiana na viongozi wa Wizara ya Ujenzi, ili kuijenga upya Temesa kuwa chombo cha matumaini, akisema hana mashaka na uwezo wake.

Mahimbali aliteuliwa Mei 3, 2026 ikiwa imepita miezi kadhaa tangu aliyekuwa na wadhifa huo, Lazaro Kilahala kusimamishwa kazi pamoja na watumishi wengine wa taasisi hiyo.

Kilahala na wenzake walisimamisha kazi Desemba 8, 2025 na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega ili kupisha uchunguzi wa tuhuma za uzembe, usimamizi dhaifu na ubadhirifu.

Viongozi mbalimbali wakiapa kiapo cha maadili kwenye hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino mkoani Dodoma Mei 6, 2026.

Katika hafla hiyo, Samia alimtaka bosi mpya wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Peter Mwasalyanda kufanya kazi na kwamba yupo katika kipindi cha uangalizi wa miezi sita.

“Tutaangalia utendaji kazi wako kabla ya kukuthibitisha kuwa mkurugenzi kamili TCRA,” amesema Samia.

Ametumia nafasi hiyo kumpongeza mkurugenzi mkuu wa zamani wa TCRA, Dk Jabir Bakari kwa kazi nzuri na sasa amembadilisha kwenda Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA).

“Nakupeleka TCAA nako kaisimamia ifanye kazi yake, hii ni sekta muhimu sana kwa usalama wa nchi yetu, usalama wa watu wanaosafiri hapa na pale kwenye anga,” ameeleza.

Cheo dhamana

Katika hatua nyingine, Rais Samia amesema vyeo ni dhamana, akisema ni dhambi kubwa mtu kupata cheo kisha ukavimba mabega na kuwa usiyegusika.

“Cheo ni dhambi kubwa ukapata cheo, ukavimbisha mabega, ukawa haugusiki wewe unanijua mimi nani who are you?” amehoji.

“Narudia tena wewe nani? Wewe ni kiumbe kama wengine, ila Mungu ameamua kushika hapo, amekupa hapo ili uwatumikie watu, kama ni sadaka yako ukiwa duniani,” amesema.

Samia amefafanua kuwa kama hutumikii watu, Mungu anajua na ana adhabu zake, akieleza kuwa Serikali inapitia tu, lakini mambo yote anaachiwa Mungu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *