Marekani. Msanii wa muziki kutoka Puerto Rico, Bad Bunny, ameendelea kuthibitisha ubunifu wake si tu kwenye muziki bali pia kwenye mitindo, baada ya kuzua gumzo katika tukio la Met Gala 2026 kufuatia mwonekano wake wa kipekee wa kizee.
Tukio hilo lililofanyika usiku wa kuamkia jana Jumanne Mei 5, 2026 jiji New York katika jumba la makumbusho la Costume Institute.
Bunny aliwasili katika maonyesho hayo akiwa na mwonekano wa mtu mzee akiwa na nywele za kijivu ‘nywele zenye mvi’, mikunjo usoni huku akitembea kwa fimbo jambo lililopelekea kuonekana wa kitofauti kabisa na kuwavutia wageni waalikwa pamoja na mashabiki.
Mwonekano huo ulikamilishwa na msanii wa prosthetics Mike Marino akiwa na timu yake ya urembo na make up.
Kwa mujibu wa maelezo yake, Bad Bunny alitumia mbinu za hali ya juu za urembo wa prosthetics akishirikiana na msanii mashuhuri Mike Marino, ili kuleta uhalisia wa uzee ulioshuhudiwa kwenye uso wake. Mbali na hilo, alivaa suti maalum ya tuxedo nyeusi aliyobuni mwenyewe kwa kushirikiana na kampuni ya mitindo ya Zara.
Suti hiyo ilinogeshwa na tai kubwa (oversized bow) iliyobuniwa na mbunifu wa zamani Charles James ya mwaka 1947 iitwayo ‘Bustle’, huku akitupia saa ya kifahari ya Cartier ya mwaka 1995.
Kwanini alivaa hivyo?
Akizungumza na Vogue alipokuwa kwenye zuria la kijani katika hafla hiyo ameeleza kilichomsukuma kutokelezea na mwonekano huo ambapo ameeleza kuwa anapendelea kufanya vitu tofauti katika maisha yake.
“Ni sehemu ya maisha yangu kujaribu kufanya kitu tofauti. Siku ya Met Gala ni siku bora ya kuchunguza, kuwa mbunifu na kujieleza kwa namna tofauti,” alisema Bunny. Katika hali ya utani, aliongeza kuwa mwonekano huo ulimchukua miaka 53 kamili kuutengeneza.
Hata hivyo baadhi ya media zinaeleza kuwa sababu kubwa iliyopelekea kuchagua mwonekano huo ni baada ya kuvutiwa na mwonekano wa msanii mwenzake The Weeknd alioutumia katika albamu ya ‘Dawn Fm’ ambapo alitumia taswira ya mtu mzee.
Mbali na mafanikio yake kwenye mitindo, Bad Bunny pia anaendelea kung’ara kwenye muziki. Wimbo wake DtMF umeweka rekodi mpya katika chati ya Hot Latin Songs baada ya kukaa nafasi ya kwanza ndani ya wiki 57, ukiivunja rekodi ya awali ya wiki 56 iliyokuwa inashikiliwa na wimbo Despacito wa Luis Fonsi na Daddy Yankee aliyemshirikisha Justin Bieber.
Aidha, msanii huyo anatarajia kuendelea na ziara yake ya kimataifa ya Debí Tirar Más Fotos World Tour, ambapo ataanza jijini Barcelona, Mei 22 na kumalizia Julai 22 mjini Brussels.