Dar es Salaam. Klabu ya Selander Bridge inatarajia kuadhimisha miaka 70 tangu kuanzishwa kwake kwa kufanya wiki maalum ya michezo, burudani na shughuli za kijamii kuanzia Mei 9 hadi 16, 2026.

Maadhimisho ya Klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 1956 na marafiki wa Kiitaliano, yanatarajiwa kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali huku mgeni rasmi akiwa Waziri Mkuu Mstaafu wa awamu ya tatu na mwanachama wa zamani, Frederick Sumaye.

Akizungumza jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk Nathaniel Mtinangi, alisema maadhimisho hayo yatakwenda sambamba na kaulimbiu ya “A Week of Thanksgiving & Merry”, yakilenga kuwakutanisha wanachama wa zamani na wa sasa pamoja na wadau wa michezo kutoka maeneo mbalimbali.

Alisema siku ya ufunguzi, Mei 9, itaanza kwa matembezi ya hisani yatakayohitimishwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, ambapo wanachama watatembelea watoto waliolazwa na kutoa msaada.

Amesema pia siku zinazofuata watakuwa na burudani na michezo mbalimbali itakayofanyika katika klabu hiyo.

“Katika wiki nzima kutakuwa na mawasilisho ya kielimu, burudani, pamoja na shughuli za kukutanisha wanachama na kujenga mtandao,” alisema Dk Mtinangi.

Aliongeza kuwa kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa Mei 15 ambapo wameandaa disco la enzi hizo kwa vijana wa zamani ambayo pia itakuwa ni burudani kwa vijana wa kisasa na Mei 16, kutakuwa na mada mbalimbali kuhusu afya, uchumi, maendeleo na mambo ya kijamii..

Akizungumzia mafanikio ya klabu hiyo, alisema yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na uaminifu, mshikamano na kujitolea kwa wanachama wake.

“Si rahisi kufikisha miaka 70, tumepitia changamoto nyingi, lakini msingi wetu mkubwa ni uaminifu na urafiki. Hii si klabu ya kibiashara, ni sehemu ya kujitolea na kushirikiana,” alisema.

Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa klabu hiyo, Dk Frank Muhamba, alisema maadhimisho hayo pia yatawakumbuka wanachama waliotangulia mbele za haki kwa kushirikisha familia zao katika shughuli mbalimbali.

Alisema mbali na matembezi ya hisani, klabu hiyo pia itatembelea wodi ya watoto wanaougua saratani na kufanya mazoezi ya pamoja kama sehemu ya kuimarisha afya na mshikamano wa wanachama.

“Msingi wa klabu hii ni urafiki na mshikamano, na tutaendelea kuuenzi kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kusaidia jamii,” alisema Dk Muhamba.

Maadhimisho hayo yanatarajiwa kuvutia wadau mbalimbali wa michezo na kijamii, huku yakitoa fursa ya kuimarisha uhusiano na kuendeleza urithi wa klabu hiyo kongwe jijini Dar es Salaam.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *