Marekani. Mwigizaji maarufu wa Marekani, Angelina Jolie, 50, ameiweka sokoni nyumba yake ya kifahari iliyopo Los Angeles, California, ambapo bei yake ni Dola29.85 milioni, wastani wa Sh77.6 bilioni.
Mshindi huyo wa tuzo ya Oscar, alinunua nyumba hiyo mwaka 2017 kwa Dola24.5 milioni kutoka kwa mtayarishaji mashuhuri wa filamu, Cecil B. DeMille.
Alifikia uamuzi huo baada ya kuachana na aliyekuwa mume wake, Brad Pitt ambaye walijaliwa kupata watoto sita – Maddox (24), Pax (22), Zahara (21), Shiloh (19), na mapacha Knox na Vivienne wenye miaka 17.
Taarifa zinaeleza kuwa Angelina amesema ataondoka mjini humo pindi tu watoto wake wadogo mapacha watakapofikisha umri wa miaka 18 hapo Julai 12, 2026.
Nyumba hiyo ya kihistoria, ipo katika eneo lenye ukubwa wa zaidi ya ekari mbili ikiwa na jumla ya vyumba sita vya kulala.
Mbali na ukubwa wake, eneo hilo linatajwa kuwa na mandhari ya kuvutia ya milima ya Hollywood Hills, na miti ya zamani zaidi ya miaka 100.
Mnamo Desemba mwaka uliopita, chanzo kimoja kilieleza kuwa Angelina alianza kuwakaribisha wanunuzi kutazama nyumba hiyo baada ya kufanya ukarabati makubwa.
Ni nyumba iliyobuniwa mwaka 1913 na mbunifu B. Cooper Corbett, na baadaye ilinunuliwa na DeMille mwaka 1916. Familia ya DeMille iliimiliki hadi mwishoni mwa miaka ya 1980.
Angelina aliwahi kueleza katika mahojiano yake ya mwaka 2024 kuwa yupo Los Angeles kwa sasa kutokana na sababu zinazohusiana na talaka yake, lakini ana mpango wa kuishi nje ya Marekani siku zijazo.
Mwigizaji huyo ambaye yeye na aliyekuwa mumewe waliachana kwa talaka Septemba 2016 baada ya miaka miwili ya ndoa na takribani miaka 11 ya kuwa pamoja, ameeleza kuwa anatarajia kutumia muda mwingi nchini Cambodia, ambako alimlea mtoto wake mkubwa Maddox mwaka 2002.
“Unapokuwa na familia kubwa, unataka wawe na faragha, amani na usalama. Nina nyumba ya kulea watoto wangu, lakini wakati mwingine mahali hapa si kama sehemu nyingine huko duniani,” alisema.
Ikumbukwe Angelina na Brad kwa mara ya kwanza walionekana pamoja hadharani na kuthibitisha uhusiano wao mwaka 2005, ikiwa ni muda mfupi baada ya Brad kutengana na aliyekuwa mkewe Jennifer Aniston.