
Unguja. Baada ya Mamlaka ya Usafiri Baharini Zanzibar (ZMA) kutangaza nauli mpya zitakazoanza kutumika Jumatatu, wananchi kisiwani hapa wameelezea masikitiko yao huku wakiiomba Serikali kuwapunguzia mzigo wananchi ambao wao ndio wanaoumia na hilo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa umma na Kitengo cha Uhusiano wa Mamlaka hiyo imesema bei hizo zinatarajiwa kuanza kutumika Jumatatu Mei 11, 2026 na kuwataka wamili wa vyombo kufuata bei iliyoanishwa na Mamlaka.
Wakizungumza na Mwananchi, wananchi hao kwa nyakati tofauti leo Ijumaa Mei 8, 2026 wamesema kinachowaumiza zaidi ni wakati ambao bei za mafuta zinaposhuka nauli za boti zikibaki hivyo hivyo bila kurudishwa bei za awali.
Mkazi wa Bububu, Ahmed Suwedi Juma amesema shida inatokea wakati ongezeko la mafuta linapopanda na nauli za usafiri hupanda, lakini yanaposhuka bei hizo zinaendelea kutumika.
“Wananchi tunatamani kueleweshwa kuhusu mwenendo huu wa bei na nashangaa wao kazi yao ni kuongeza tu sio kushusha yaani bei ya mafuta ikikaa sawa wao ndio bei yao haibadiliki,” amesema.
Ahmed amesema kutokana na hali ilivyo kuna uwezekano mkubwa kwa nauli hizo za boti kufikia kiwango cha Sh100,000 na hapo ndipo yanapotengenezwa mazingira ya kumuua masikini kisaikolojia.
Mwengine, Mkazi wa Kama, Maryam Ally Hamdani amesema, kimbilio la wanyonge na Watanzania wengi ni usafiri wa boti ambao ndio uwezo wao, kwa hali hiyo hawatakuwa na sehemu ya kujitetea upande wao.
“Sisi wananchi kimbilio letu ni wapi? hatuna uwezo wa nauli za ndege ndio sababu ya kutumia usafiri wa baharini, mambo yanakuwa magumu kila siku,” amesema Maryam.
Amesema, Ongezeko la Sh5,000 kwa mwananchi wa kawaida ni kubwa sana na Mamlaka husika ingewaonea huruma wananchi wake wenye hali za chini.
Imrani Hassan Hasuni amesema, huko ni kuonea abiria Zanzibar, kwa sababu hizo boti zinauwezo wa kununua mafuta na nauli ikabaki ya Sh35,000 na siyo Sh40,0000.
Anasema, kawaida za vyombo usafiri vinakimbilia kupandisha nauli za boti kupata faida za juu lakini kwenye jambo lakushusha hawataki kuliewa.
Pia, amesema wananchi wanaweza kukubaliana na hilo kwa wakati ila wanaiomba Serikali mafuta yakishuka na bei zishuke kwa sababu kila mwaka nauli za boti zinapanda.
Mwengine, Hassan Saleh Mahmoud ameiomba Serikali kutokana na kipindi hichi kigumu cha mafuta iondoshe kodi kwenye kila tiketi moja kwa kuwaonea huruma wananchi ambao ndio waathirika na hilo.
“Tunaiomba Serikali iondoshe kodi kwenye kila tiketi moja kwa kutuonea huruma wananchi ambao ndio tunaopata tabu na kuumia,” amesema
ZMA imetoa ongezeko la bei ya tiketi ya boti kutoka Zanzibar hadi Dar es Salaam itakuwa 40,000 kutoka Sh35,000 kwa daraja la chini na nusu tiketi itauzwa kwa Sh20,000 na bei ya Flying horse itakuwa 22,000 kutoka Sh20,000 na nauli za boti kutoka Unguja hadi Pemba zitakuwa kama ilivyo Sh40,000 na Pemba hadi Tanga Sh30,000.