Dar es Salaam. Shirika la Uwakala wa Meli Tanzania (Tasac) imeanza kusaka suluhu ya foleni ya malori jijini Dar es Salam kwa kujadili changamoto ya uanzishwaji na uendeshaji wa bandari kavu jijini hapo.

Tasac imetaja changamoto ya uwepo wa bandari kavu ni ongezeko la msongamano wa magari katika barabara, ucheleweshaji wa upatikanaji wa mizigo kwa wateja, kuongezeka kwa gharama kwa wateja na uwezo mdogo wa bandari kavu hizo kushindwa kuhudumia mizigo mingi.

Kwa mujibu wa Tasac, kumekuwa na ongezeko la shehena katika bandari ya Dar es Salaam na changamoto iliyopo ndani ya bandari hiyo haijawahi kuongezeka.

Leo Mei 8,2026 shirika hilo amesema limekutana na wadau kutoka mamlaka za Serikali kujadili uanzishwaji na uendelezwaji wa bandari kavu jijini Dar es Salaam ambapo kutatolewa maazimio ya kukabiliana na utitiri wa bandari kavu na changamoto zake ikiwemo foleni.

Akizungumza kwenye mkutano huo Mkurugenzi Mkuu wa Tasac, Mohamed Salum wingi wa makontena ya mizigo inayoingia nchini inachangia kwa kiasi kikubwa hali hiyo.

“Uwezo wa bandari ya Dar es Salaam katika kuhifadhi makontena ukiwa kwenye uwezo wake wa asilimia 100 unachukua makontena 28,000 kwa mara moja lakini kitaalamu uhudumiaji wa malori ndani ya bandari haupaswi kuzidi asilimia 65,zaidi ya hapo ufanisi wa bandari unashuka,”amesema.

Mkurugenzi Mkuu wa TASAC Mohamed Salum akizungumzia uanzishwaji na uendelezwaji wa bandari kavu Dar es Salaam.

Salum amesema kwa mwezi mmoja pekee makontena yanayoingia nchini ni 110,000  na ili yahudumiwe lazima yatoke nje ya bandari ndio maana ya umuhimu wa uwepo wa bandari kavu.

Pamoja na kiwango hicho cha makontena, Salum amesema kiwango cha bandari kavu zilizopo Dar es Salaam uwepo wake kwa ujumla haiwezi kuchukua makontena zaidi ya 37,000.

“Bado kuna uwezo mdogo wa kuhifadhi makontena, pia tuna changamoto makontena yakiingia nchini inabidi tena yatoke na kwa takwimu za Desemba mwaka jana, makontena yaliyotoka nchini ni 47,000 kwahiyo kuna bandari kavu inayohudumia makontena ya ndani na mengine ya nje,”amesema Salum.

Amesema uwepo wa bandari kavu ni jambo la muhimu kuwezesha bandari nchini kufanya kazi.

Salum amesema kulingana na takwimu za Tasac uwezo wa bandari ya Dar es Salaam kila mwaka inakua kwa zaidi ya asilimia 16 na hadi kufikia 2030 uwezo wa bandari kuhudumia makontena utaongezeka mara mbili.

Akizungumzia usafirishaji wa makontena nje ya nchi, Salum amesema katika makontena 110,000 yanayoingia bandari ya Dar es Salaam nusu yake yanasafirishwa nje ya nchi na mengine asilimia 90 yanabaki Dar es Salaam kwa mwezi.

Kwa upande wake Mkurugenzi Udhibiti na Usimamizi wa Huduma za Usafiri Majini Nelson Mlali amesema dhumuni la kuanzishwa kwa bandari kavu ni kupunguza msongamano wa makasha bandarini na zaidi ya asilimia 80 ya bandari hizo zipo Dar es Salaam.

“Sababu ya uwepo wa bandar hizo nyingi Dar es Salaam ni kutokana na uwepo wa idadi kubwa ya watu hivyo kusababisha bidhaa nyingi zinazoagizwa kutoka nje ya nchi kupata soko Dar es Salaam na uwepo wa viwanda vingi kuliko sehemu nyingine,”amesema.

Mlali amesema wilaya ya Temeke ndio yenye bandari kavu nyingi 74 sawa na asilimia 64.3, Kigamboni 13 sawa na asilimia 11.3, Ilala 22 sawa na asilimia 19.1, Ubungo bandari kavu 2 sawa na asilimia 1.7 na Kinondoni 4 sawa na asilimia 3.5.

“Ili kuleta ufanisi wa Bandari ya Dar es Salaam na kupunguza kero wakati Serikali ikiendelea na hatua mbalimbali za uwekezaji ni muhimu wadau wote tukashirikiana kukabiliana na changamoto zilizopo kwa kuzingatia kanuni na sheria zilizopo za uanzishwaji wa bandari kavu,”amesema Mlali.

Kwa upande wake Mkurugenzi Msaidizi wa Usafiri wa Majini Wizara ya Uchukuzi Mussa Shashula amesema Serikali inaendelea kuwekeza kwenye bandari kavu ili kuongeza ufanisi wa bandari ya Dar katika kuhudumia ongezeko la makontena

Amesema matokeo ya uwekezaji huo umeonekana kutokana na ongezeko la mizigo kwneye bandari hiyo kuongezeka kutoka tani milioni 18 mwaka 2021/22 hadi tani milioni 32 mwaka 2024/25.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *