Dar es Salaam. Majeruhi mwingine katika vurugu za Lupaso, Vikawe wilayani Kibaha mkoani Pwani, amefariki dunia hivyo kufanya idadi ya vifo vilivyotokana na vurugu hizo kufikia vinne.

Majeruhi huyo aliyetambulika kwa jina moja la Nassoro, amefariki dunia majira ya saa sita mchana leo Mei 8, 2026 akiwa anapatiwa matibabu katika Hospitali ya Mkoa ya Tumbi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase amesema leo Mei 8, 2026 kuwa aliyefariki dunia ni kati ya majeruhi wawili ambao hali zao zilikuwa mbaya.

“Amefahamika kwa jina moja tu la Nassoro. Amefariki muda si mrefu, ni miongoni mwa waliokuwa majeruhi wawili ambao walikuwa hawaongei,” amesema Kamanda Morcase.

Mbali na hilo, RPC Morcase amesema upepelezi wa tukio unaendelea na mmiliki wa eneo anayeshikiliwa wanaendelea na mahojiano naye, upelelezi ukikamilika atapelekwa mahakamani.

Katika vurugu hizo zilizosababishwa na mgogoro wa ardhi kwenye eneo la Lupaso, watu waliotajwa kuwa mabaunsa walivamia alfajiri ya kuamkia Mei 6, 2026 na kubomoa nyumba za wakazi kabla ya kuanza mapambano baina yao wakitumia nyundo, visu na mapanga.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa huo, Shaban Ally Shaban, familia 10 zimekosa makazi baada ya nyumba 20 kubomolewa na mabaunsa. Kati ya nyumba hizo, 10 zilikuwa na watu waliokuwa wanaishi ndani yake huku nyingine 10 wahusika wakiwa bado hawajahamia.

Alisema siku ya tukio takriban watu 300 walifika Lupaso kwa usafiri wa mabasi madogo sita aina ya Toyota Coaster, wakiwa na mapanga na nyundo wakivunja nyumba za wananchi.

“Wakati huo wananchi pia walikuwa wanapiga filimbi kuitana, ndipo zikatokea vurugu kubwa zilizosababisha vifo vya wale mabaunsa watatu. Wananchi wakajeruhiwa na ukatokea uharibifu wa mali kadhaa ikiwamo nyumba,” amesema.

Katika vurugu hizo mabaunsa watatu walipoteza maisha siku hiyo huku wanaume 15 wakijeruhiwa, wakiwamo mabaunsa na wakazi wa Lupaso, sambamba na kutokea uharibifu wa mali.

Leo mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa wa Vikawe, Shaban Ally Shaban, alipoulizwa iwapo anamfahamu raia kwenye eneo hilo anayefahamika kwa jina la Nassoro, amesema hakuna mwananchi kwenye eneo lake anayefahamika kwa jina hilo na akasema huenda naye ni miongoni mwa mabaunsa.

Mabaunsa hao wanatajwa kuagizwa na mwenye eneo hilo kufuatia mgogoro wa ardhi uliokuwepo baada ya wananchi kuuziwa maeneo kati ya mwaka 2008 hadi 2023, na Februari 2025 kugundulika walitapeliwa baada ya mwenye eneo halali kujitokeza.

Mgogoro huo uliamuliwa na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Nickson John maarufu Niki wa Pili, na kufikiwa maridhiano kuwa eneo lipimwe na waliojenga wamlipe mwenye eneo halali kwa kiwango cha Sh3,000 kwa kila mita ya mraba.

“Huo ndio muafaka uliofikiwa na pande zote mbili kuuridhia. Baada ya eneo kupimwa, mwenye eneo alikataa maridhiano na alfajiri ya Mei 6, 2026 mabaunsa kama 300 walivamia wakiwa kwenye mabasi madogo sita aina ya Toyota Coaster,” amesema mwenyekiti huyo wa mtaa.

Amesema wananchi waliitana na kuibuka vurugu kubwa kati ya mabaunsa na wananchi, hali iliyosababisha vifo, majeruhi na uharibifu wa mali. Ameongeza kuwa eneo hilo hadi sasa lipo chini ya ulinzi wa polisi wenye silaha za moto na mabomu ya machozi.

Akizungumzia maisha ya wananchi waliobomolewa makazi yao na kupewa hifadhi kwenye nyumba ambazo ujenzi wake haujakamilika, Shaban amesema Serikali ya mtaa kupitia wadau mbalimbali imechangisha fedha na kuwasaidia chakula.

“Familia zilizokosa makazi ni 10. Kila moja imepewa kiroba cha unga cha kilo 10 na Sh20, 000 kwa ajili ya chakula,” amesema.

Amesema mwanafunzi wa darasa la saba aliyepoteza vifaa vyake vya shule amesaidiwa kurejea darasani baada ya uongozi wa mtaa kumnunulia vifaa vipya, na leo Ijumaa amerejea shuleni.

“Mwanafunzi huyo, begi lake lenye madaftari, sare na vifaa muhimu vya masomo vilipotea wakati familia yake ikikimbia vurugu hizo,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *