Arusha. Hali ya simanzi imetanda katika Kata ya Kimandolu jijini Arusha baada ya mtoto mwenye umri wa miaka 14, Shaban Saddick kufariki dunia akidaiwa kunyongwa na jirani.

Tukio hilo limetokea juzi Mei 9, 2026 saa 2 usiku.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo amethibitisha kwa njia ya simu kutokea kwa tukio hilo huku akisema tayari upelelezi wa tukio hilo umeanza.

“Tumeanza upelelezi wa tukio hilo ikiwamo kuwahoji watu kadhaa wanaohusishwa na tukio hilo, hivyo upelelezi ukikamilika tutachukua hatua zaidi,” amesema.

Hata hivyo, alipoulizwa idadi ya watu wanaowashikilia, alikata simu, na alipopigiwa tena simu iliita bila kupokewa na ujumbe pia haukujibiwa.

Akizungumzia tukio hilo, dada wa marehemu, Saada Saddick amesema juzi saa moja jioni akiwa anatoka vibandani kununua mkaa, alimwona dada wa kazi wa jirani akimuita mdogo wake, akimshawishi waende kula, baada ya kuingia ndani ya geti wakafunga kwa komeo.

“Mimi niliwaona wakibembelezana, nikawauliza kuna nini lakini hawakunijibu, wakacheka wakaingia ndani ya geti na kulifunga kwa komeo.

“Hata sikuwajali, niliingia ndani na kuwasha mkaa na kuendelea kupika, kisha nikatenga na kuamua kwenda kumuita saa tatu usiku,” amesema.

Amesema alikwenda kugonga geti hilo kwa muda mrefu huku akiita bila kujibiwa na kuamua kwenda kuchukua kisu kutengua komeo.

“Wakati nimerudi kugonga kidogo ili nitengue komeo, jirani wa pembeni alinisaidia kufungua na kuondoka zake.

“Nilipoingia ndani nikiwa naongea na simu nikamkuta mdogo wangu amekaa chini huku shingo imening’inia kwenye kamba ya kuanikia nguo,” amesema.

Amesema awali alidhani mdogo wake anamtania, hivyo alimpiga mguu akimwambia aache utani, lakini hakuitika.

“Yule msichana aliyekuwa naye, ananiuliza mdogo wako ndiyo anakuwaga hivyo? Nikamuuliza anakuwaje? Hajibu bali anaweka mikono mifukoni akiwa ananiangalia.

“Nilimsogelea mdogo wangu na kumshika mkono kutaka kumvuta, ndipo nikashangaa mikono ni ya baridi sana na hana nguvu. Nilitumia kile kisu kukata kamba iliyokuwa shingoni nikidhani bado ni utani, ndiyo nikashangaa akaanguka chini akiwa na majeraha shingoni,” amesema.

Saada amesema alimuuliza tena dada huyo amemfanyaje mdogo wake bila kupata majibu, hivyo alimwomba amsaidie kumuweka mgongoni bila mafanikio.

“Kila ninachomuuliza hajibu, nilimuomba anisaidie kuniweka mgongoni, pia alikataa, akakimbilia ndani kwao na kufunga mlango.”

Amesema alimbeba mdogo wake hivyo hivyo kwa shida na kutoka nje ya geti na kuanza kupiga kelele.

“Watu wengi walitoka na wazazi wangu pia walikuja na kujionea hali halisi, ndipo wakaita polisi wakawachukua watuhumiwa hao na kuondoka nao,” amesema.

Mama wa marehemu, Amina Hassan amesema usiku huo akitoka kwenye msiba alimsikia mtoto wake mkubwa akipiga kelele kabla ya kumkimbilia na kukuta yuko pembeni ya mwili wa mdogo wake.

“Polisi walikuja akawaeleza ilivyokuwa na wakaondoka wote kwenye gari la polisi, yeye akarudi.

“Tunachoshangaa huyo kaka aliyekuwa na huyo msichana wa kazi, ambaye ni ndugu wa mwenye nyumba, ameachiwa, wakati tunashuku kwa umri wa dada wa kazi na mtoto wangu kutekeleza hilo peke yake ingekuwa ngumu maana wangeweza kutoshana nguvu.

“Tena mbaya zaidi, taarifa mpya zinakuja eti inadaiwa mtoto wangu hajanyongwa bali amekunywa sumu,” amesema.

Amesema shaka kubwa waliyonayo ni kauli ya mtoto kunywa sumu wakati ana majeraha makubwa shingoni yanayoashiria kunyongwa.

“Hata kama angekuwa amekunywa sumu, bado wanahusika maana ni wao wamempa. Mtoto ametoa wapi sumu ya kunywa?

“Ninaamini kuna jambo nyuma ya kifo cha mwanangu, ameonekana na majeraha shingoni na watu tunaowahisi mmoja yuko nje,” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina juu ya kifo cha mwanaye.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *