Ni miongo miwili (miaka 20) sasa ambapo BRAC Tanzania imekuwa mshirika muhimu na aliyejizatiti katika kuwezesha na kutafuta suluhu za umasikini pamoja na ukosefu wa usawa nchini.
Hii ni kutokana kwamba, ikiwa na nusu ya idadi ya watu wenye umri wa chini ya miaka 30, Tanzania nchi iliyojaa fursa nyingi lakini karibu nusu ya watu wake wanaishi kwa kipato cha chini ya dola 3 za Kimarekani kwa siku.
Na ndiyo maana, tangu mwaka 2006, BRAC Tanzania imekuwa mashirika muhimu wa Serikali na jamii nchini, hususani wanawake na vijana kwa kuwawezesha kupambana na umasikini pamoja na ukosefu wa usawa.
Tangu kuanzishwa kwake nchini Bangladesh zaidi ya miaka 50 iliyopita, BRAC imekuwa ikifanya kazi na jamii kushughulikia sababu na dalili za umaskini uliokithiri na ukosefu wa haki za kijamii.
Klabu ya vijana walio katika rika la balehe inayotekelezwa na BRAC Maendeleo Tanzania.
Historia ya BRAC inanza mwaka 1972, ilipoanza kama mpango mdogo wa misaada baada ya vita vya ukombozi vya Bangladesh ambapo kwa sasa ni moja ya mashirika makubwa zaidi ya maendeleo duniani yaliyoanzishwa katika nchi za Kusini, ikishirikiana na zaidi ya watu milioni 145 katika bara la Asia na Afrika.
BRAC inaamini kwamba umasikini upo katika hali tofauti hivyo unahitaji nguvu za pamoja katika kukabiliana nao. Hii ndiyo sababu BRAC inaunganisha kwa pamoja elimu, afya, ujumuishi wa kifedha, shughuli za kujikimu, usalama wa chakula na biashara ndogo kama mfumo mmoja wa ikolojia uliyobuniwa ili kuleta mabadiliko ya kudumu.
Mfumo huo unaonekana katika historia ya miaka 20 ya BRAC nchini Tanzania ambapo hadi sasa takribani wakulima 200,000 sawa na asilimia 65 kati yao wakiwa wanawake, wameboresha uzalishaji wa mazao ya kilimo na lishe katika kaya zao tangu washirikiane na BRAC.
Aidha, wakulima wadogo wamewezeshwa kwa kupatiwa pembejeo bora za kilimo zikiwemo mbegu, mbolea, viuatilifu, chakula cha mifugo pamoja na kupata huduma za kifedha na mtandao wa uhakika wa masoko.
Upatikanaji wa huduma za kifedha pia ni sehemu muhimu ya mkakati wa BRAC katika kulata maendeleo jumuishi, ukienda sambamba na programu zake za kijamii ili kuchochea mabadiliko endelevu na kuwasaidia watu kujikwamua kutoka kwenye umaskini.
BRAC Tanzania Finance Limited ndiyo taasisi kubwa zaidi ya huduma ndogo za kifedha nchini, ikiwasaidia watu waliopo nje ya mifumo rasmi ya kifedha kupata huduma bora za kifedha na zana zinazowasidia kuwekeza kwa ajili ya wao wenyewe, familia zao na jamii zao kwa ujumla. Hadi Machi 2024, BRAC Tanzania Finance Limited ilikuwa na matawi 184 nchi nzima, ikihudumia karibu wateja 360,000, ambapo asilimia 98 ni wanawake.
Mabadiliko endelevu yanakwenda sambamba na ushirikiano hivyo BRAC inashirikiana na Wizara ya Afya na Maendeleo ya Jamii kuimarisha elimu ya awali, jambo lililopelekea kupatikana kwa mwongozo wa walezi na mtaala unaozingatia michezo kwa watoto wenye umri wa miaka 2 hadi 4, ambavyo vyote baadaye vilipitishwa na kutumika katika ngazi ya kitaifa.
Zana hizi zinawapa walezi na waelimishaji msaada wa vitendo kwa maendeleo ya utambuzi na kijamii ya watoto katika hatua muhimu zaidi za ukuaji katika maisha yao.
Mwaka 2020, BRAC ilianzisha taasisi yake ya kwanza ya kibiashara ya kijamii nchini kwa lengo la kuwawezesha watoto wengi kuwa na mwanzo bora kupitia mtandao wa wajasiriamali wadogo ambao wamejengwa kupitia mfumo wa BRAC wa kujifunza kupitia michezo. Mfumo huu umeundwa ili kuifanya elimu ya awali kuwa bora na inayopatikana kwa gharama nafuu.
Mfumo huu unafanya kazi kwa kutoza ada katika vituo vinavyohudumia familia zenye kipato cha kati na kutumia mapato hayo kupunguza gharama katika vituo vinavyohudumia familia zenye kipato cha chini pamoja na kitengo cha kujifunzia kinachotembea kilichowezesha kusogeza elimu ya awali karibu kabisa na jamii.
Leo hii, kuna vituo 13 vya kujifunzia vya Angaza jijini Dar es Salaam ambavyo si tu vimeboresha upatikanaji wa elimu ya awali bali pia vimetengeneza fursa za ajira na kusaidia wajasiriamali wazawa hasa wanawake kuendesha na kukuza biashara endelevu ndani ya jamii zao.
Pamoja na programu ya maendeleo ya awali ya watoto, BRAC imepanua wigo wake wa kuwaandaa vijana kuingia kwenye soko la ajira. Mwaka 2020, taasisi hiyo ilizindua programu ya majaribio jijini Dar es Salaam ikiwapa wanafunzi wa shule za sekondari, hususani wasichana wenye umri wa miaka 14 hadi 24, stadi za kidijitali na za maisha.
Washiriki hawakupatiwa tu ujuzi, bali pia uelewa wa mwelekeo na ujasiri wa kuufuata, pamoja na uelewa mzuri wa afya na haki zao. Baada ya kukamilisha mafunzo hayo, washiriki walipata nafasi ya kuingia kwenye programu nyingine tofauti inayotumia nguvu ya michezo kutoa elimu ya stadi za maisha kwa wasichana balehe na wanawake vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 24 katika jamii zenye kipato cha chini.
Programu hii imesaidia kujenga hali ya kujiamini, uongozi na ujuzi wa kufanya maamuzi na kuwawezesha wasichana wengi kubaki shuleni, kuepuka ndoa za utotoni na kukabiliana na changamoto za kijamii kwa uwezo mkubwa.
Kwa pamoja, mikakati hii miwili imewafikia zaidi ya vijana 3,000 moja kwa moja, huku lengo likiwa ni kuongeza idadi hii na kufungua fursa zaidi katika ulimwengu wa teknolojia na ajira kwa vijana.
Ikijikita katika ushahidi wa vitendo ndani ya miongo mitano ya kuwawezesha vijana, BRAC Tanzania ilianza programu hii yenye matokeo makubwa zaidi mwaka 2022. Katika utekelezaji wake, ilishirikiana na wasichana balehe na wanawake vijana kutoka katika jamii zilizo hatarini ikiwa na lengo kuu la kuboresha ubora wa maisha yao.
Kwa kupitia mazingira salama na yenye furaha, Angaza Learning Centre inakuza kujiamini kwa watoto, ustawi, na utayari wa kujifunza.
Programu hii ni sehemu ya mkakati wa ‘Young Africa Works’ unaofadhiliwa na Mastercard Foundation, unaolenga kusaidia vijana milioni 30 wa kiafrika ambapo asilimia 70 kati yao wakiwa wanawake vijana kupata kazi zenye staha ifikapo mwaka 2033.
Kwa Tanzania, programu hii itawafikia zaidi ya wasichana balehe na wanawake vijana 700,000 katika kipindi cha miaka saba ijayo, kwa kuwatengenezea mazingira salama na bora ya kujifunzia, ujasiriamali unaozingatia umri, ajira na mafunzo ya stadi za maisha, pamoja na zana za kuanzisha na kukuza biashara zao wenyewe.
Programu hii inafanya kazi na familia, jamii na wadau mbalimbali ili kuweka mazingira wezeshi yanayochochea mabadiliko chanya ya kijamii na kitabia kwa wasichana na wanawake vijana.
Kazi hii yote inafanyika kwa lengo kubwa moja; Kuweka jamii katikati ya maendeleo kwa ajili ya kukuza uwezo wa kujitegemea, ili ziweze kuwa vichocheo vya mabadiliko yao wenyewe.
Katika kipindi ambacho mifumo ya maendeleo inasuasua, misaada haitabiriki na changamoto zinaendelea kuongezeka, BRAC Tanzania inatoa taswira ya kipekee kwamba mabadiliko ya kweli hayatoki nje, yanajengwa kwa uvumilivu, kwa uhalisia, kutoka ndani ya jamii ambazo zinayahitaji, kuyamiliki na hatimaye kuyaongoza.