Kwa muda mrefu maeneo ya nyanda za malisho yamekuwa yakitazamwa kama yaliotengwa na yasio na umuhimu, licha ya kuwa na mifumo ikolojia muhimu na chanzo cha riziki kwa takriban watu bilioni mbili duniani, Pamoja na kuhifadhi theluthi moja ya hewa ya kaboni duniani.

Imechapishwa:

Dakika 4 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Lakini sasa wadau wa mazingira, watunga sera, watafiti, wataalam na wawakilishi kutoka jamii za wafugaji baranai Afrika sasa wanatoa wito wa maeneo ya nyanda za malisho na jamii za wafugaji kutambuliwa.

Katika kongamano la siku mbili lililofanyika jijini Nairobi nchini kenya, kuhusu mustakabali wa nyanda za malisho na jamii za wafugaji, Dkt Eliane Ubalijoro, mkurugenzi mtendaji wa CIFOR-ICRAF, alisema

Nyanda za malisho ni miongoni mwa maeneo yanayopuuzwa, licha ya fursa zilizopo kwenye maeneo hayo. Maeneo haya yanaweza kuwa kiungo muhimu katika kuhakikisha usalama wa chakula na kukabili tabianchi.”

Dr Eliane Ubalijoro – Mkurugenzi Mtendaji Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Misitu na Kilimo cha Msituni CIFOR-ICRAF

Aidha Katika kongamano hilo, washiriki pia walitoa wito wa kubadili uelewa kuhusu maeneo ya nyanda za malisho, vilevile namna maeneo hayo yanafadhiliwa na kuthaminiwa. Mkurugenzi mkuu wa taasisi ya kimataifa ya utafiti kuhusu mifugo ILRI Profesa Appolinaire Djikeng anasema “ushahidi uko wazi, asilimia 66 ya ardhi Afrika ni nyanda za malisho, na mamilioni ya watu wanategemea maeneo hayo kujipatia riziki.”

Aidha Profesa Djikeng anasisitiza haja ya kubadilisha dhana kuhusu maeneo ya nyanda za malisho. “Kinachohitajika ni kubadili mitazamo na kuyatazama maeneo haya kama fursa. Kuna mambo mengi mataifa yanaweza kunufaika kutoka kwenye maeneo nyanda za malisho na nafikiri tunahitaji kubadili dhana na lazima tutambue na kuwekeza katika mifumo ya ufugaji.” 

Miongoni mwa maeneo muhimu ni namna data kutoka kwenye jamii za wafugaji inawezakutumika  kuboresha usimamzi wa nyanda za malisho. 

Joshua Laizer, mfugaji anayejishusisha na masuala ya usimamizi wa nyanda za malisho kutoka nchini Tanzania, anasema,

Tuna data nyingi, kama vile idadi ya mifugo, idadi ya wafugaji wenyewe, lakini pia katika ngazi ya kijamii kuna mambo mengine ambayo wanasayansi wanaweza wasichukulie kama data. Kuna taarifa kuhusu njia za asili za ufugaji, mipango ya matumizi bora ya ardhi za asili.”

Joshua Laize – Wakili na Mfugaji kutoka Tanzania

Wanawake na kumiliki ardhi

Katika hatua nyingine, wadau wametaka wanawake wafugaji kupewa kipaumbele na kusaidiwa katika kupata haki hasa linapokuja suala la umiliki wa mali.

Wito huu umetolewa wakati ambapo katika mataifa mengi ya ukanda wa Afrika Mashariki, licha ya sera na sheria kutambua haki za wanawake katika kumiliki mali kama vile ardhi na nyumba, kuna changamoto katika utekelezaji wake.

Mfano, barani Afrika, ardhi hutumiwa sana na wanawake na wasichana, hata hivyo mchango wao umeendelea kutotambuliwa na hata kutofadhiliwa.

Wanawake wafugaji na wakulima wameendelea kukabiliwa na changamoto ya kurithi na kumiliki ardhi kutokana na mifumo na urithi wa sheria za kikoloni, unaotokana namna rasilimali zinagawanywa na namna mabadiliko ya sheria yanavyotekelezwa.

Anna Ngito, wakili na mwanaharakati wa masuala ya jinsia (Katikati) akiwa katika moja ya mijadala.
Anna Ngito, wakili na mwanaharakati wa masuala ya jinsia (Katikati) akiwa katika moja ya mijadala. ©Global Landscapes Forum

Katika mkutano wa ‘Nyanda za Malisho” mwaka 2026, wanaharakati, wafugaji na wakulima wanawake walijadili na kubainisha changamoto na vipaumbele ambavyo nchi zinapaswa kufanyia kazi kuleta mabadiliko ya kweli katika mifumo ya sheria.

Aidha suala la namna ufadhili wa kifedha unaweza kuwa shirikishi  na thabiti kusaidia haki za wanawake katika kumiliki wa ardhi lilijadiliwa kwa kina, wajumbe wakikubaliana kimsingi kuwa kuna haja ya kushirikisha mamlaka na wanaume katika kutambua haki hizo.

Akizungumza na mhariri wa idhaa hii, Anna Ndiko, wakili na mwanaharakati wa masuala ya jinsia kutoka Tanzania, anasema nchi zimepiga hatua katika kutengeneza sheria rafiki, akitolea mfano marekebisho ya sheria ya ardhi ya hivi karibuni ambayo yalimpa mwanake haki ya kumiliki ardhi.

Pamoja na hatua hizo za kimafanikio kuna suala zima la kuchumi, bado wanawake kwenye uchumi tuko nyuma. Na kwenye uchumi tunamaanisha umiliki wa mali na fedha, fedha ni pamoja na njia za uzalishaji na vyanzo vya mapato, ambapo kipato kile ndicho kinaweza kumsaidia mwanamke kuweza kujiendeleza”.

Anna Ndiko – Wakili na Mwanaharakati wa Masuala ya Jinsia

Anna ameongeza kuwa “unapokuwa na ardhi utahitaji kulima, utahitaji kupalilia, utahitaji kuvuna, vyote hivyo vinahitaji nguvu kazi kubwa ambayo ni mwanamke peke yake anaweza kuhitaji kuleta wafanyakazi kumsaidia, na kwasababu hiyo kwakuwa hana uwezo wa kufikia vyanzo vya mapato, basi hawezi kuwa katika kiwango kimoja cha ushindani na wanaume.”

Pamoja na changamoto zote zinazowakabili wanawake wakulima na wafugaji duniani, Anna anasema anaamini jamii bado ina nafasi kubwa ya kutoa mchango wake kuhakikisha wanawake wanainuliwa kiuchumi, jamii kuelimishwa kuachana na mila na tamaduni potofu kuhusu wanawake na wasichana. 

Wito unazidi kutolewa kwa jukumu la jamii za wafugaji kutambuliwa katika kutunza maeneo haya ambayo yanategemewa na takriban watu bilioni mbili duniani wakiwemo jamii za wafugaji.

Kuelekea mikutano ya Umoja wa mataifa ya tabianchi na bioanuai, washiriki walibadilishana mawazo katika nyanja tofauti kama vile, teknolojia, ubunifu, Suluhu zinazoweza kutekelezeka na hatua zinazohitajika  katika usimamazi na uhifadhi wa maeneo ya nyanda za malisho.

Aidha ofisi inayosimamia mkataba wa umoja wa Mataifa wa kupambana na ueneaji wa jangwa (UNCCD) ilitoa ripoti kuhusu ufugaji na nyanda za malisho mwezi Mei tarehe 21 mwaka 2024, ambapo ilisisitiza maendeleo ya sera, mipango mkakati ya uhifadhi, nyanda za malisho endelevu na urejeshaji wa maeneo husika. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *