Kishapu. Katika jitihada za kuimarisha haki za familia na kupunguza migogoro ya ndoa katika jamii, wananchi wa kijiji cha Mwagembe, kata ya Mwataga wilayani Kishapu mkoani Shinyanga wamehamasishwa kusajili na kurasimisha ndoa zao za kimila ili zitambulike kisheria ili kuimarisha ustawi wa familia.

Akizungumza leo Mei 14, 2026 na Mwanasheria wa serikali Hussein Mandari katika mkutano wa hadhara, uliofanyka Kata ya Mwataga Halmashauri ya wilaya ya Kishapu, amesema kuwa bado wananchi wengi wanaishi katika ndoa za kimila ambazo hazijasajiliwa rasmi,

“Bado wananchi wengi wanaishi katika ndoa za kimila ambazo hazijasajiliwa rasmi jambo linaloweza kusababisha changamoto za kisheria na migogoro ya kifamilia pindi matatizo yanapotokea, usajili wa ndoa ni hatua muhimu ya kulinda na kuimarisha ustawi wa familia” amesema Mandari.

Pia ameongeza kuwa “Ndoa za kimila zinarasimishwa kupitia maofisa tarafa waliopo katika maeneo yenu, ili ziweze kutambulika kisheria na kuwapa haki wanandoa na watoto na kurahisisha utatuzi wa migogoro ya kifamilia” ameongeza Mandari.

Naye mkazi wa Kijiji cha Mwagembe, Kata ya Mwataga Said ameeleza kuwa wanandoa wanapaswa kujenga utamaduni wa mazungumzo na kuheshimiana ili kupunguza migogoro ndani ya familia na kuepuka kusambaza siri za ndani,

“Kuna baadhi ya wanandoa wakikosana ndani wanaanza kutoa maneno nje ya familia, hii inaonesha kutoheshimiana kuna umuhimu wa kukaa chini na kuzungumza changamoto zetu kwa kusikilizana, hii itapunguza migogoro ya kifamilia katika vyombo vya sheria katika jamii,” amesema Said.

Aidha Ofisa Ustawi wa Jamii Halmashauri ya Kishapu, Mwajuma Abeid ameongeza kuwa, toka wameanza kutoa huduma ya msaada wa kisheria kesi nyingi zimekuwa zikihusishwa na migogoro ya kifamilia ikiwemo masuala ya mirathi.

“Kitu kinachokwamisha utatuzi wa masuala ya mirathi, tumegundua wananchi hawajasajiri ndoa zao za kimila, hii inaleta ugumu wa kufikia muafaka kwa sababu hawatambuliki kisheria kama wanandoa,” ameeleza Mwajuma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *