Uchunguzi wa awali wabaini utambulisho wa miili 12 iliyopatikana pwani ya Matrouh, MisriUchunguzi wa awali wabaini utambulisho wa miili 12 iliyopatikana pwani ya Matrouh, Misri

Vyanzo rasmi vya Misri vimefichua kwamba miili 12 iliyopatikana kwenye boti ya mpira siku ya Alkhamisi nje ya pwani ya kijiji cha Abu Ghleila katika mji wa Sidi Barrani ni ya vijana wa Misri kutoka majimbo 5 nchini humo.

Vyanzo katika Mkoa wa Matrouh wa Misri vimeeleza kwamba uchunguzi wa awali kuhusu tukio hilo ulibaini kuwa vijana hao, ambao ni kutoka majimbo ya Assiut, Giza, Qalyubia, Beheira na Dakahlia, walikuwa kwenye safari ya uhamiaji isiyo rasmi kutoka eneo la Tajoura mashariki mwa Libya.

Taarifa zinasema kwamba vijana hao walikwama baharini baada ya kukosa chakula na maji, na wakafa mmoja baada ya mwingine ndani ya boti ya mpira, ambayo haikuwa na vifaa vinavyohitajika kwa ajili ya safari kama hiyo.

Vyanzo vinasema, wachunguzi wamehitimisha kwamba wahajiri wengine kadhaa waliokuwa ndani ya boti hiyo huenda walianguka baharini, kwani tabia ya madalali wa uhamiaji haramu katika maeneo hayo inahusishwa na kusafirisha watu wengi kadiri iwezekanavyo kwenye boti hizo ili kupata faida maradufu.

Mji wa Sidi Barrani upo kaskazini magharibi mwa Misri kwenye pwani ya Mediterania kando ya mpaka wa Libya, na kiutawala uko chini ya gavana wa Misri wa Matrouh.

Mamlaka husika ya Misri ilihamishia miili ya vijana hao kwenye Hospitali Kuu ya Marsa Matrouh mara tu baada ya wakazi wa kijiji cha Abu Ghleila kutoa taarifa kuhusu kupatikana wa boti hiyo ya mpira. Miili hiyo ilikuwa imeoza na katika hali mbaya, na ilionekana kwamba vijana hao walifariki dunia kutokana na ukosefu wa chakula kwa kipindi cha kati ya siku 10 na 15.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *