Katika jamii nyingi za Kiafrika, mwanaume amejengwa kuonekana kama nguzo imara isiyotetereka kirahisiKatika jamii nyingi za Kiafrika, mwanaume amejengwa kuonekana kama nguzo imara isiyotetereka kirahisi

Katika jamii nyingi za Kiafrika, mwanaume amejengwa kuonekana kama nguzo imara isiyotetereka kirahisi. Tangu utotoni, wengi hufundishwa kuwa kulia, kueleza maumivu au kuomba msaada ni udhaifu.

Matokeo yake, wanaume wengi hubeba mizigo ya kihisia kimyakimya huku wakijitahidi kuonekana wenye nguvu mbele ya familia na jamii. Lakini nyuma ya ukimya huo, kuna maelfu ya wanaume wanaopambana na msongo wa mawazo, upweke na sonona bila kuwa na sehemu salama ya kueleza wanachopitia.

Majukumu ya maisha, changamoto za kiuchumi, presha ya kuhudumia familia na matarajio makubwa kutoka kwa jamii huongeza mzigo mkubwa wa kihisia kwa wanaume wengi. Tofauti na wanawake ambao mara nyingi hupata nafasi ya kueleza hisia zao na kuungwa mkono kirahisi, wanaume wengi huogopa kuzungumza kwa hofu ya kubezwa, kudharauliwa au kuonekana dhaifu.

Kwa mujibu wa taarifa mbalimbali za afya duniani, wanaume wengi huathirika na changamoto za afya ya akili lakini hushindwa kutafuta msaada mapema. Wapo wanaotabasamu mchana huku usiku wakipambana na mawazo mazito wakiwa peke yao.

Ukimya huu umechangia kuvurugika kwa mahusiano ya kifamilia, kupungua kwa ufanisi kazini na wakati mwingine kupoteza maisha kutokana na sonona na msongo wa mawazo usiotibiwa.

Wataalamu wa saikolojia wanaeleza kuwa kuficha hisia kwa muda mrefu huongeza madhara ya afya ya akili. Binadamu yeyote anahitaji kusikilizwa, kueleweka na kupata msaada wa kihisia. Hata hivyo, mfumo wa kijamii bado unamnyima mwanaume nafasi hiyo kwa kuamini kuwa mwanaume halisi hapaswi kulalamika wala kuonesha udhaifu.

Ni muhimu sasa jamii kubadili mtazamo wake kuhusu afya ya akili ya mwanaume. Nguvu ya kweli si kuficha maumivu, bali ni uwezo wa kutambua changamoto na kutafuta msaada inapohitajika. Tunahitaji mazingira ambayo mwanaume anaweza kusema “nimechoka”, “nina mawazo” au “nahitaji msaada” bila kuhukumiwa.

Afya ya akili ya mwanaume si suala binafsi pekee, bali ni suala la familia, jamii na maendeleo ya taifa. Kadri tunavyoendelea kupuuza ukimya huu, ndivyo tunavyoendelea kupoteza utulivu wa familia, furaha ya jamii na wakati mwingine maisha ya wanaume wenyewe.

#AzamTVUpdates
✍Imeandaliwa na Halia Abdallah
Mhariri | John Mbalamwezi

(Feed generated with FetchRSS)

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *