
Balozi wa Cuba katika Umoja wa Mataifa amesisitiza haki ya nchi yake kujilinda dhidi ya uwezekano wowote wa uvamizi wa kijeshi kutoka Marekani, kwa mujibu wa sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Katika mahojiano na shirika la habari la Russia la TASS, Ernesto Sobrón Guzmán amepinga madai ya Marekani yanayoionyesha Cuba kuwa tishio, akisema wazi kwamba “Cuba si tishio kwa usalama wa taifa wa Marekani. Mtu yeyote anayesema vinginevyo anasema uongo.”
Amesisitiza haki halali ya Cuba kujilinda iwapo kutatokea uvamizi wowote wa kijeshi
Kauli hizo zimekuja kama jibu kwa ripoti tata ya tovuti ya Axios, chombo cha habari kilicho karibu na Rais Trump wa Marekani, iliyowanukuu maafisa wasiojulikana wa ujasusi wa Marekani wakidai kuwa Cuba imepata zaidi ya droni 300 za kivita katika miaka ya hivi karibuni, hasa kutoka Russia na Iran.
Ripoti hiyo ilidai kuwa maafisa wa jeshi la Cuba wamejadili uwezekano wa kutumia droni hizo dhidi ya malengo ya Marekani, yakiwemo kambi ya majini ya Guantanamo Bay iliyo chini ya udhibiti wa Marekani, manowari za kijeshi za Marekani, na hata mji wa Key West, Florida ya kusini, endapo kutatokea ongezeko la mivutano.
Maafisa wa Marekani, ingawa wanakuza kupita kiasi kile walichokiita “tishio,” walilazimika kukiri kuwa Cuba haiwakilishi hatari ya karibu, na kwamba uwezo wake wa kijeshi hauwezi kulinganishwa na matukio ya kihistoria kama mzozo wa makombora wa mwaka 1962.
Maafisa wa cuba, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Bruno Rodríguez, wamekosoa vikali ripoti ya Axios wakisema ni sehemu ya madai bandia ili kuhalalisha vikwazo vilivyoongezwa, vita vya kiuchumi, na uwezekano wa hujuma ya kijeshi chini ya kampeni ya shinikizo la juu inayotekelezwa na utawala wa sasa wa Marekani.
Hali hii inaendelea kuakisi mtindo wa sera za Marekani za kulenga mataifa huru yanayopinga ushawishi wake wa kibeberu, kwa kuunda visingizio vya kisiasa vya kuyashinikiza.
Cuba, kama Iran, kwa muda mrefu imekuwa ikikabiliwa na vikwazo haramu vya Marekani, mzingiro wa kiuchumi, na jitihada za kuyumbisha uthabiti wake kwa lengo la kudhoofisha mamlaka yake na misingi yake ya mapinduzi ili isalimu amri mbele ya ubabe wa Washington.
