
Arusha. Serikali imejipanga kuharakisha kukamilika kwa Sera ya matumizi ya Akili Unde (AI) ili ianze kutumika rasmi na kutoa mwongozo wa matumizi ya teknolojia hiyo nchini.
Hayo yameelezwa leo Jumanne Mei 19, 2026 na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sayansi na Teknolojia kutoka Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dk Haroun Makandi, wakati akizungumza katika kongamano la kitaifa kuhusu matumizi ya QR Code na AI lililofanyika jijini Arusha.
Amesema lengo la kuharakisha kupatikana kwa sera hiyo ni kukuza matumizi ya AI, kuboresha na kuimarisha bunifu na kwamba kwa sasa ipo katika hatua ya rasimu ndani ya Serikali.
“Kupitia kongamano hili, tunatarajia kupata mapendekezo yenu yatakayosaidia kupata sera bora ya matumizi ya AI na QR code. Sera hiyo kwa sasa iko hatua za awali serikalini, sisi tutajitahidi kurekebisha ili isonge mbele na kuanza kutumika,” amesema.
Amesema matumizi ya AI yanapaswa kuzingatia maadili ili teknolojia hiyo ilete manufaa kwa jamii na taifa kwa ujumla.
“Matumizi ya AI lazima yazingatie maadili kwani ukichanganya matumizi sahihi ya AI, maadili na uwezo wa mtu binafsi, mabadiliko yanayoweza kupatikana ni makubwa mno,” amesema.
Dk Makandi, amesema kwa kuzingatia mfumo wa sera ya AI, bado Afrika Mashariki haipo vizuri, ingawa Tanzania imepiga hatua kwenye miundombinu na elimu.
“Ndiyo maana mwaka jana kulikuwa na wasilisho la mwongozo wa masuala ya AI, sasa tunataka hilo lisonge mbele ili lichangie kwenye mfumo madhubuti wa sera ya matumizi ya AI pamoja na QR Code,” amesema.
Amesema lengo la Serikali ni kuimarisha uwezo wa vijana na taasisi za elimu katika matumizi ya teknolojia mbalimbali za kisasa ili kukuza umahiri, maarifa na kuibua vijana wabunifu.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Scan Code Tanzania, Faustine Mgimba, amesema kongamano hilo limebebwa na kauli mbiu “Ubunifu Tanzania kwa kutumia teknolojia za QR Code na Akili Unde kwa mageuzi jumuishi ya kidijitali.”
Amesema lengo ni kuhakikisha maendeleo ya teknolojia yanawanufaisha Watanzania wote bila kumuacha mtu nyuma.
“Tunatambua kupitia QR Code na AI tunaweza kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma, kupanua fursa za biashara na kuboresha utendaji kazi katika sekta binafsi na Serikali,” amesema.
Mgimba, amesema dunia ipo katika mageuzi makubwa ya kidijitali huku AI ikiendelea kubadilisha namna watu wanavyoishi, kufanya biashara na kutoa huduma.
“Leo QR Code imekuwa sehemu muhimu katika biashara mtandaoni, huduma za kifedha, usafirishaji na mifumo ya udhibiti,” amesema.
Amesema Tanzania ina nafasi ya kuwa kitovu cha ubunifu wa teknolojia barani Afrika, kutokana na mazingira mazuri yaliyowekwa.
