Waziri Mkuu ashtukia kuuzwa dhamana za wakopajiWaziri Mkuu ashtukia kuuzwa dhamana za wakopaji

Dodoma. Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba amesema mfumo wa benki wa kuuza dhamana za wakopaji bila kuangalia kiasi cha deni lililobaki, kinaumiza watu na akataka utaratibu utazamwe.

Dk Mwigulu pia ametaja kero kwa wakopaji ambapo mfumo wa benki unamtaka anayekopa mamilioni ya fedha kuwa na makaratasi lundo sawa na mkopaji wa Sh2 milioni jambo suala linalowasukuma  wengine wakakope kwenye mikopo kausha damu kusiko na mizunguko mingi.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo jana Jumanne Mei 19, 2026 wakati akihutubia kwenye kilele Cha maadhimisho ya miaka 20 ya Bodi ya usimamizi wa Stakabadhi za ghala (WRRB) jijini Dodoma.

Dk Mwigulu amesema kuuza dhamana ya mkopaji aliyoweka kwa thamani ya deni lililobakia inaumiza wengi na inafikirisha kwa kiasi kikubwa.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, akionesha Mkakati wa Uhamasishaji Matumizi ya Mfumo wa Stakabadhi za Ghala, mara baada ya kuuzindua, alipofunga Maadhimisho ya Miaka 20 ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma Mei 19, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

“Mfano kuna mtu alikopa Sh37 milioni kwa dhamana ya trekta, alilipa ikabaki Sh10 milioni halafu benki wakaenda kuuza trekta zima, hii ni dhuluma,” amesema Dk Mwigulu.

Amemwomba Gavana wa Banki Kuu ya Tanzania (BoT) kuweka mfumo na dirisha la mkopo kwa kutumia mali zinazohamishika akisisitiza kuwa lazima vyeti vya wanafunzi vitumike kwa dhamana.

Akizungumzia mfumo wa stakabadhi za ghala amesema ni wakati kwa Watanzania kutoogopa mageuzi kwani mtindo wa kuaminiana umepitwa na wakati.

Waziri Mkuu amesema waliofanikiwa sehemu kubwa ni waliopita kwenye mifumo sahihi na si njia za mkato.

Hata hivyo, ametaja changamoto ya umbali wa yalikojengwa maghala na wakulima kukopesha mazao yao lakini wanachelewa kupata malipo ni vikwazo vinavyopelekea mfumo kuonekana ni mbaya.

Waziri Mkuu ametaja suluhisho la matatizo hayo ni kujenga maghala karibu na wakulima na kuwa na malipo ya awali kwenye ununuzi wa mazao ili waanze kupunguza makali ya maisha wakati wakisubiri malipo ya jumla.

Waziri Mkuu Dk Mwigulu Nchemba, akizungumza wakati alipokuwa akifunga Maadhimisho ya Miaka 20 ya Bodi ya Usimamizi wa Stakabadhi za Ghala (WRRB) katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini Dodoma Mei 19, 2026. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu

Awali, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga ametaja alichokiita jambo la msingi kwenye mfumo ni kuwa na uhakika wa masoko.

Waziri Kapinga amesema ndani ya masoko hayo kunakuwa na bei shindani ambayo inatoa faida kubwa hivyo wakulima na wadau wanapaswa kuutetea kwa nguvu zote.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *