
Washington. Marekani imetangaza mashtaka ya mauaji dhidi ya Rais wa zamani wa Cuba, Raúl Castro, hatua inayotajwa kuwa ni mwendelezo wa kampeni kali ya Marekani dhidi ya serikali ya kikomunisti ya taifa hilo la visiwani.
Hati hiyo ya mashtaka, iliyotangazwa jana Mei 20, 2026, imezidi kuzorotesha uhusiano kati ya mahasimu hao wa muda mrefu tangu enzi za Vita Baridi, huku Rais wa Marekani, Donald Trump, akiendelea kushinikiza mabadiliko ya utawala nchini Cuba, ambako chama cha kikomunisti kimeendelea kushika madaraka tangu mapinduzi ya mwaka 1959 yaliyoongozwa na marehemu Fidel Castro.
Mashtaka dhidi ya Raúl Castro pamoja na marubani watano wa kijeshi wa Cuba yanatokana na tukio la mwaka 1996 ambapo ndege za kivita za Cuba zilitungua ndege zilizokuwa zikiendeshwa na kundi la wakimbizi wa Cuba waliokuwa uhamishoni.
Raúl Castro mwenye umri wa miaka 94 anakabiliwa na shtaka moja la kula njama za kuwaua raia wa Marekani, mashtaka manne ya mauaji na mashtaka mawili ya uharibifu wa ndege.
Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, Castro alionekana hadharani nchini Cuba mapema mwezi huu na hakuna ushahidi unaoonyesha ameondoka nchini humo au atasafirishwa kwenda Marekani kujibu mashtaka hayo.
Ni nadra kwa Marekani kufungua mashtaka ya jinai dhidi ya viongozi wa kigeni. Hatua hiyo ni mfano mwingine wa juhudi kali za utawala wa Trump kupanua ushawishi wa Marekani katika Ukanda wa Amerika ya Kusini.
“Kuanzia pwani za Havana hadi mfereji wa Panama, tutatokomeza nguvu za uhalifu, vurugu na ushawishi wa mataifa ya kigeni,” Trump alisema akiwa katika hafla ya Chuo cha Walinzi wa Pwani mjini New London, Connecticut, mapema Jumatano iliyopita.
Akizungumza mjini Miami katika hafla ya kuwaenzi waathirika wa tukio la mwaka 1996, Kaimu Mwanasheria Mkuu wa Marekani, Todd Blanche, hakujibu moja kwa moja iwapo jeshi la Marekani litamkamata Castro.
Hata hivyo, Blanche alisema anaamini Castro siku moja atafikishwa mahakamani kujibu mashtaka hayo.
“Kibali cha kukamatwa kwake tayari kimetolewa, hivyo tunatarajia atafika hapa kwa hiari yake au kwa njia nyingine,” alisema huku akishangiliwa na maofisa wa serikali pamoja na Wamarekani wenye asili ya Cuba waliohudhuria hafla hiyo.
Kupitia ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa X, Rais wa Cuba, Miguel Díaz-Canel, alisema Cuba ilichukua hatua halali kulinda mipaka yake kwa kuzidungua ndege hizo. Alisema mashtaka hayo yanaonekana kuwa sehemu ya mkakati wa kuhalalisha hatua za kijeshi dhidi ya Cuba, jambo alilosema litakuwa kosa kubwa.
“Huu ni mchezo wa kisiasa usio na msingi wowote wa kisheria,” alisema Díaz-Canel.
Mashtaka hayo yamekuja miezi michache baada ya kukamatwa kwa Rais wa Venezuela, Nicolás Maduro, Januari 3, 2026 ili kujibu mashtaka ya biashara ya dawa za kulevya mjini New York. Maduro ambaye ni mshirika wa karibu wa Havana alikana mashtaka hayo.
Ushawishi Amerika ya Kusini
Kuongezeka kwa ushawishi wa Marekani katika Amerika ya Kusini, kunakoonekana kupitia kukamatwa kwa Maduro, kunatajwa kuwa sehemu muhimu ya urithi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Marco Rubio, ambaye ni mtoto wa wahamiaji wa Cuba na anatajwa kuwa mmoja wa wanaoweza kuwania urais mwaka 2028.
Mpinzani wake mkubwa ndani ya chama cha Republican, Makamu wa Rais, JD Vance, amekuwa akipinga kwa muda mrefu Marekani kujihusisha na vita vya mataifa mengine.
Chini ya Trump, Marekani imeendelea kuibana Cuba kiuchumi kwa kutishia kuiwekea vikwazo nchi zinazoiuzia mafuta, hatua iliyosababisha kukatika kwa umeme na kuzidisha mgogoro mkubwa wa kiuchumi nchini humo.
Mapema Jumatano, Rubio aliipatia Cuba msaada wa dola milioni 100 huku akiilaumu serikali ya taifa hilo kwa kukosekana umeme, chakula na mafuta. Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Bruno Rodríguez Parrilla, aliutaja msaada huo kuwa wa kinafiki kutokana na athari kubwa za vikwazo vya Marekani.
Cuba ilivyodungua ndege
Raúl Castro aliyezaliwa mwaka 1931 alikuwa mmoja wa viongozi wakuu pamoja na kaka yake Fidel Castro katika vita vya msituni vilivyomng’oa madarakani dikteta aliyeungwa mkono na Marekani, Fulgencio Batista.
Baada ya kuingia madarakani, Fidel Castro aliingia ushirikiano na Umoja wa Kisovieti na kutaifisha mali pamoja na biashara zinazomilikiwa na Wamarekani. Marekani imeendelea kuiwekea Cuba vikwazo vya kiuchumi tangu wakati huo.
Raúl Castro pia alihusika katika kushindwa kwa uvamizi wa Bay of Pigs uliopangwa na Marekani mwaka 1961 na baadaye akawa Waziri wa Ulinzi kwa miongo kadhaa. Alimrithi kaka yake kama rais mwaka 2008 kabla ya kujiuzulu mwaka 2018, lakini anaendelea kuwa na ushawishi mkubwa kisiasa nchini humo.
Wakati wa tukio la mwaka 1996, Raúl Castro alikuwa Waziri wa Ulinzi. Ndege mbili ndogo zilizokuwa zikiendeshwa na kundi la wakimbizi wa Cuba lenye makao yake Miami, Brothers to the Rescue, zilitunguliwa na kuwaua wote waliokuwamo ndani.
Kundi hilo lilisema lilikuwa likiwatafuta wakimbizi wa Cuba waliokuwa wakikimbia taifa hilo kwa kutumia mitumbwi. Fidel Castro aliwahi kusema jeshi la Cuba lilitekeleza maagizo ya kutungua ndege zote zinazoingia katika anga ya Cuba, lakini akasema Raúl Castro hakutoa amri maalumu ya kushambulia ndege hizo.
Baadaye, Shirika la Kimataifa la Usafiri wa Anga lilihitimisha kuwa ndege hizo zilitunguliwa katika anga ya kimataifa.
Picha za wanaume wanne waliouawa Carlos Costa, Armando Alejandre Jr., Mario de la Peña na Pablo Morales zilionyeshwa wakati wa hafla hiyo mjini Miami.
Wamarekani wenye asili ya Cuba walikusanyika nje ya jengo la Freedom Tower mjini Miami, ambalo lilitumika kama kituo cha wakimbizi wa Cuba miaka ya 1960, kabla ya hafla hiyo kuanza.
“Tulikuwa tukisubiri kwa miaka mingi jambo hili litokee,” alisema Bobby Ramirez, mwanamuziki mwenye umri wa miaka 62 ambaye aliondoka Cuba mwaka 1971 akiwa na miaka saba.
