Chadema yatoa msimamo Tume ya Jaji Lila, wadau watahadharishaChadema yatoa msimamo Tume ya Jaji Lila, wadau watahadharisha

Arusha/Dar. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimesema hakitashirikiana na Tume ya uchunguzi wa masuala ya jinai iliyoundwa na Rais Samia Suluhu Hassan, kikidai kuwa haina uhuru na inalenga kuwashughulikia waliokuwa wakidai Katiba mpya na uchaguzi huru na haki.

Akizungumza katika mkutano mkuu maalumu wa kanda uliowakutanisha viongozi waandamizi wa chama hicho Kanda ya Kaskazini jijini Arusha jana Mei 21, 2026, Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika amesema chama hicho kinaona tume hiyo ni mwendelezo wa Tume ya Jaji Mohamed Chande ambayo tayari ilielekeza lawama kwa watu waliokuwa wakitoa kaulimbiu za “No Reforms No Election” na “Oktoba Tunatiki”.

Katika taarifa ya Ikulu ya Mei 18, 2026, Rais Samia Suluhu Hassan aliunda Tume ya Uchunguzi wa Jinai wa matukio ya Oktoba 29, 2025 na kumteua Jaji Shaban Lila kuiongoza. Hatua hiyo ilitokana na mapendekezo ya Jaji Chande baada ya kuwasilisha ripoti yake kwa Rais Samia.

Katika mapendekezo yake, Jaji Chande alipendekeza Tume mpya (ya jinai) ifanye uchunguzi wa kina wa makosa ya jinai yaliyojitokeza wakati na baada ya uchaguzi huo ili kuwezesha uwajibikaji wa kisheria.

Katika Tume hiyo, makamishna watatu, Gad Mjemmas, Awadh Bawazir na Aishiel Sumari waliteuliwa kuendesha uchunguzi huo.

Hata hivyo, Mnyika amesema baada ya uchaguzi wa mwaka 2025, Chadema kupitia Kamati Kuu ilitangaza kuwa hakukuwa na uchaguzi halali na kuitaka Serikali kufuta uchaguzi huo na kurudia upya   baada ya kupatikana katiba mpya na tume huru ya uchaguzi.

Kuhusu uwajibikaji wa matukio ya uvunjifu wa amani yaliyotokea, Mnyika amesema chama hicho kilitaka kuundwa kwa chombo huru chenye watu wa kitaifa na kimataifa kuchunguza mauaji na madhila yaliyojitokeza kabla na baada ya uchaguzi.

Mnyika amebainisha kuwa badala ya kufanya hivyo, Serikali iliunda Tume ya Jaji Chande ambayo baadaye ilieleza kuwa ilikuwa ikikusanya taarifa pekee na kupendekeza kuundwa kwa tume nyingine ya kuchunguza masuala ya jinai.

Akizungumzia maelezo ya Jaji Chande katika ripoti yake, Mnyika amesema Tume ya Jaji Chande, iliibua hoja za madai ya katiba mpya, kutokuwa na uchaguzi huru na haki pamoja na kaulimbiu za “No Reforms No Election” na “Oktoba Tunatiki” kama vichocheo vya matukio yaliyotokea Oktoba 29, 2025, akisisitiza uwajibikaji ulenge waliohusika na ukiukwaji wa haki za binadamu badala ya waliodai haki.

“Badala ya kushughulikia walioua, waliosababisha mauaji kutokea na waliotoa amri za watu kuuawa, wameamua kushughulikia vichocheo,” amesema.

Kwa mujibu wa Mnyika, hatua hiyo inaonyesha kuwa tume mpya imeundwa kwa nia ya kuwashughulikia wanaharakati, viongozi wa dini na Chadema badala ya kutafuta ukweli kuhusu mauaji yaliyotokea.

“Tunasema hii tume ina nia ovu na dhamira ovu. Ni mwendelezo wa ripoti ya uongo ya Jaji Chande. Lakini wale waliohusika na mauaji, waliosababisha mauaji kutokea, waliokwamisha mchakato wa katiba mpya, waliotoa amri za watu kuuawa wamewekwa kwenye vyanzo na tume iliyoundwa inashughulikia mkondo wa kukwepesha haki.

“Nataka niseme hapa msimamo wetu ni ule tuliotoa wakati wa tume ya Jaji Chande, aliyeunda tume hii ya pili ni Rais yuleyule na ametumia sheria ile ya uchaguzi ambapo kifungu kilichounda hii tume kinasema Rais anaweza kuifanya ripoti kuwa ya siri. Sheria hiyo inatoa mamlaka kwa mtu mmoja kufanya ripoti kuwa siri yake, jambo ambalo halikubaliki,” amesema.

Mnyika pia amehoji uteuzi wa wajumbe wa tume hiyo, akidai baadhi yao hawana historia ya kusimamia haki kutokana na uamuzi wao ya awali ya kimahakama.

Mwelekeo wa chama

Kutokana na sababu hizo, Mnyika amesisitiza kuwa Chadema haitatoa ushirikiano kwa Tume hiyo kama ambavyo haikushiriki katika Tume ya Jaji Chande, huku akikiri kuwa chama hicho kinatambua kuwa tume hiyo ya kijinai inaweza kutumia mamlaka ya kisheria kuwaita watu kwa lazima au kuitisha nyaraka, lakini chama kitajadili hatua hizo endapo zitafikiwa.

Amesisitiza kuwa msimamo wa Chadema unabaki kuwa lazima kwanza kuundwe chombo huru kitakachochunguza matukio hayo kwa uwazi ili ukweli, haki na uwajibikaji vipatikane.

“Tunatambua hii kwa sababu ni tume ya kijinai itapewa kisheria mamlaka ya ziada ya kuita watu kwa lazima kutumia njia nyingine za kisheria kuita watu kwa lazima hata kama hawataki na kuitisha nyaraka kwa lazima hata kama taasisi hazitaki ikifikia hatua hizo tutakaa kwenye vikao.

“Kama watatuita kama watuhumiwa tutakaa vikao vya chama kuamua namna ya kushughulika na jambo hilo lakini tunaendelea na msimamo wetu, Tanzania hii kabla ya chochote kingine lazima kuundwe kwanza chombo huru cha kuchunguza kwa uhuru tupate ukweli, haki, uwajibikaji kabla yna baada ya uchaguzi,” amesema.

Tahadhari ya wadau

Akizungumzia mtazamo huo, mwanadiplomasia mkongwe, Profesa Benson Bana anatahadharisha juu ya mivutano hii akisisitiza umuhimu wa kutumia njia za kisheria kwa wasiokubaliana na Tume hiyo huku akiitaka Tume kutenda haki ili kulinda tunu za umoja na mshikamano wa Kitaifa.

“Tanzania bado ni moja, tunu zetu za amani, umoja na mshikamano bado tunazo. Tunaweza kuwa tofauti zetu za dini, vyama na makabila lakini bado tuko wamoja.

“Tume anazounda Rais ni kwa mujibu wa sheria na msingi wa uchunguzi wanaokwenda kuufanya Tume ya Jaji Lila utatokana na uchunguzi wa Chaji Chande, watakaokutwa na kesi za kijinai watapendekezwa kufikishwa kwenye vyombo vya sheria. Hivyo kikubwa sheria ifuatwe na haki itendeke,” anasisitiza.

Bana amewataka wale wanaoipinga Tume hii kutumia misingi ya kisheria wakijua misimamo yao inaweza kuwasha moto, akiweka wazi kuwa zipo sheria za kufuata kwa jambo ambalo mtu au taasisi haikubaliani nalo.

Wakili Dk Onesmo Kyauke anasema ili kuepusha mgawanyiko kwenye jamii, Tume inatakiwa itende haki, wale watakaokutwa na hatia hata kama watakuwa ndani ya Serikali watajwe. Hii itaondoa mpasuko.

“Wale wanaoikosoa Tume nao wanayo haki kusema hivyo, bila kufanya hivyo sidhani kama hata maridhiano ya kitaifa yatafanikiwa,” anasema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *