Drake atema nyongo kupitia albamu zake tatuDrake atema nyongo kupitia albamu zake tatu

Canada. Rapa kutokea Canada anayefanya shughuli zake Marekani, Drake (39) ni kama ameamua kutema nyongo katika albamu zake tatu mpya ambazo ameziachia kwa wakati mmoja wiki hii, kitu ambacho hakuna aliyetarajia.

Drake, mkali wa kibao cha God’s Plan (2018), albamu tatu alizoachia ni Iceman (2026), Habibti (2026) na Maid of Honour (2026) zikiwa na jumla ya nyimbo 43, hatua iliyomfanya rapa huyo sasa kuwa na jumla ya albamu 11.

Albamu ya Iceman ina nyimbo 18 zenye muda wa saa 1 na dakika 8, Maid of Honour ina nyimbo 14 zenye dakika 45, huku Habibti ikiwa na nyimbo 11 zenye dakika 36.

Vilevile cover za albamu hizo zimeonyesha ubunifu mkubwa ambapo cover ya Maid of Honour ina picha ya mama yake Drake akiwa kijana, Iceman inaonyesha gloves za Michael Jackson, huku Habibti ikiwa na picha ya mwanamke aliyefunikwa mwili mzima kwa bandeji na kuachiwa macho tu.

Tangazo la ujio wa albamu hizo lilitolewa kupitia livestream iliyorushwa kwenye channel yake ya YouTube ambapo alitoa hard drive tatu, kisha yakafutia maandishi yaliyosomeka; I made this so that I could make this.

Video ilianza kwa kuonyesha mandhari ya kuvutia ya jiji la nyumbani kwao la Toronto pamoja na mnara maarufu wa CN Tower.

Wimbo wa kwanza kutoka katika albamu ya Iceman uitwao ‘Make Them Cry’’, video yake unamuonyesha Drake akiwa katika hali ya tafakari, akizungumzia ugonjwa wa saratani ambao baba yake anakabiliana nao.

Na katika livestream hiyo, pia alionekana DJ Akademiks ambaye alitoa ujumbe uliowalenga wakosoaji wa Drake.

Kwenye video ya wimbo ‘Dust’, mchekeshaji Shane Gillis alionekana akiwa ndani ya gari la polisi huku mtoto wa Drake, Adonis akiwa anaendesha gari hilo.

Hata hivyo, katika albamu hiyo Drake alijumuisha baadhi ya nyimbo zake ambazo tayari zilikuwa zimeshatoka ambazo ni; National Treasures na Which One aliyomshirikisha Central Cee.

Katika wimbo na video ya ‘Ran to Atlanta’, ambao Drake ameshirikiana na Future pamoja na Molly Santana, humu ameamua kujibu diss ya Kendrick Lamar aliyoitoa kupitia ngoma yake maarufu, Not Like Us (2024).

Kwa upande wa mashairi ya baadhi ya nyimbo za albamu hizo, Drake amesikika akiwachana vikali wapinzani wake katika rapa hasa Kendrick Lamar, huku pia akisisitiza kuwa nafasi yake katika Hip Hop bado ipo pale pale.

Mkali huyo wa kibao cha Hotline Bling (2016), alienda mbali zaidi akiwakosoa wanaotumia takwimu za mauzo ya muziki katika majukwaa ya kidijitali (digital streaming) kupima mafanikio ya wasanii.

Vilevile imebainika kuwa katika wimbo wake ‘Make Them Pay’, Drake amemchana DJ Khaled kwa ukimya wake kuhusu mateso wanayopitia watu wa Gaza licha ya kuwa ana asili ya Palestina.

Albamu hizo zimekuja baada ya ugomvi wake mkubwa na Kendrick Lamar uliotikikisa ulimwengu wa Hip Hop mwaka 2024.

Bifu hilo lilimalizika baada ya Lamar kuachia ngoma ya diss (Not Like Us) iliyofanya vizuri hadi kushinda tuzo mbili za Grammy 2026.

Mafanikio ya diss hiyo ni kama yalishusha heshima ya Drake, hivyo kupitia albamu hizi tatu mpya (Iceman, Habibti na Maid of Honour) anataka kulisafisha jina lake kufuatia mijadala iliyokuwa ikiendelea dhidi yake baada ya bifu hiyo na Lamar.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *