Unguja. Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wamesema licha ya jitihada kubwa zinazofanywa na Serikali kutangaza utalii, bado tija haijaonekana hivyo inataka kuongeza jitihada kupanua soko la utalii.
Wametoa kauli hiyo leo Mei 23, 2026 wakati wakichangia nakadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Barazani Chukwani Unguja Zanzibar.
Katika mchango wake, mwakilishi wa Wingwi, Kombo Mwinyi Shehe (ACT Wazalendo) amesema ipo haja Serikali kupitia wizara hiyo kujitafakari upya kuona njia wanazotumia kama zinaleta tija iliyokusudiwa.
“Jitihada kubwa zinafanyika kutangaza utalii, lakini ipo haja kufikiria njia zinazotumika maana hatuoni matokeo makubwa kama inavyozungumzwa na kutangazwa,” amesema Kombo.
Hoja kama hiyo pia imetolewa na mwakilishi wa Wawi, Bakar Hamad Bakar ambaye amesema kuwa nchi nyingi duniani ambazo zinakuza utalii zinatumia miji yao, tamaduni zao kuvutia watalii hivyo lazima na Zanzibar ijikite katika mipango hiyo.
“Haya ndio maeneo yanayoongeza uzito kwa hiyo bila kukaa imara tunaweza kupigwa bao lazima tujitofautishe na wengine ili watalii waendelee kuchagua kuja hapa Zanzibar,” amesema.
Mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad akichangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti ya Wizara ya Utalii na Mambo ya Kale Barazani, Chukwani Unguja Zanzibar.
Amesema watalii hawezi kuja ikiwa hakuna mambo ya tofauti ambayo yatawavutia kwa hiyo ipo haja kuonesha utofauti katika utoaji wa huduma.
Ameshauri, “Ili tufanikiwe katika hayo lazima tutangaze vivutio vyetu kwa kutumia vyombo vya habari vya ndani na vya nje. Bado tunahitaji kufikia masoko makubwa zaidi huko duniani.”
Ameeleza pia kuhusu kutokuwapo na kumbi za mikutano kwani bado itakuwa kazi ngumu kuwaleta wageni wa kimataifa kufanyia mikutano Zanzibar. “Hatuwezi kutengeneza kituo cha kimataifa kama hatuna kumbi za mikutano.”
Amesema kumekuwapo na mipango ya muda mrefu kujenga kumbi lakini haitekelezeki hivyo akataka kujua lini jambo hilo litafikiwa.
Mwakilishi wa Amani, Masoud Amour Masoud amesema lazima wizara iongeze jitihada katika kutangaza utalii hususani katika vyakula vya asili kwani wageni wakija wanataka kuvijua lakini kwa sasa mapishi ya vyakula hivyo hayajatangazwa vya kutosha.
Kwa upande wake mwakilishi wa Pandani, Profesa Omar Fakih Hamad (ACT Wazalendo) amesema licha ya kuwa sekta ya utalii ndio inatazamwa kutoa mchango mkubwa katika uchumi wa Taifa lakini inasikitisha kiasi kidogo cha bajeti kinachotengwa katika sekta hiyo.
Amesema bado haijaonesha mkakati mahususi kuhakikisha utalii unaendelea kukuza uchumi, huku akisema bado jitihada za kuhifadhi maeneo ya kale hazionekani kwa ukubwa wake kama inavyotakiwa hivyo jitihada inatakiwa kuongezwa.
Amesema kama Serikali imekusudia kukuza utalii basi haina budi kuongeza fedha katika sekta hiyo tofauti na ilivyo sasa.
“Bado kuna maeneo hayajatangazwa na hayajafikiwa hivyo yanapaswa kuibuliwa kama mapango ili kuongeza kasi katika kutangaza utalii na kuongeza mapato,” amesema.
Naye Mwakilishi wa Pangawe Ali Suleiman Ameir (CCM) amesema bado Zanzibar inaendelea kujifunza katika utalii kwa hiyo lazima jitihada ziongezwe kufikia malengo yanayokusudiwa.
