Teknolojia inavyowanasua vijana janga la ajiraTeknolojia inavyowanasua vijana janga la ajira

Dar es Salaam. Wakati ukosefu wa ajira rasmi ukiendelea kuwa miongoni mwa changamoto zinazowakabili vijana nchini, kizazi kipya kimeibuka na mbinu mbadala za kujipatia kipato kupitia mitandao ya kijamii, biashara za mtandaoni na kazi za kujitegemea, hali inayozidi kubadili taswira ya soko la ajira Tanzania.

Kuanzia TikTok, Instagram, YouTube hadi WhatsApp, mitandao ya kijamii imekuwa soko jipya la ajira lisilo rasmi linalowapa vijana nafasi ya kuuza bidhaa, kutangaza biashara, kutengeneza maudhui na hata kufanya kazi za masoko bila kuwa na ofisi wala mtaji mkubwa.

Katika mazingira ambayo ushindani wa ajira umeendelea kuwa mkubwa, simu janja sasa zimegeuka kuwa sehemu ya kazi, studio za kurekodia na maduka ya mtandaoni kwa vijana wengi wa Kitanzania.

Mwananchi imezungumza na vijana mbalimbali wanaotumia teknolojia kujitengenezea kipato, wengi wakisema walilazimika kubadili mtazamo baada ya kuona ajira rasmi zinakuwa ngumu kupatikana.

Kelvin Joseph, mkazi wa Mbagala, Dar es Salaam ni miongoni mwa maelfu ya vijana nchini wanaogeukia uchumi wa kidijitali kama njia mbadala ya kujinasua katika changamoto ya ukosefu wa ajira rasmi.

Tofauti na miaka michache iliyopita alipokuwa akizunguka na bahasha za maombi ya kazi kutoka ofisi moja hadi nyingine, sasa simu hiyo ndiyo ofisi yake na chanzo chake kikuu cha kipato.

Kijana huyu alianza kwa kuposti video za vichekesho TikTok kama burudani, lakini baadaye zikageuka kuwa chanzo kikuu cha mapato.

Anasema hakuwahi kufikiria jambo aliloanza kama burudani lingegeuka kuwa kazi inayomwingizia fedha za kujikimu.

“Nilianza kwa kuposti video kwa ajili ya kujifurahisha tu. Baadaye watu wakaanza kuzisambaza, wanaonifuatilia wakaongezeka, leo hii ndiyo kazi yangu kamili,” anasema Kelvin.

Kwa Neema Said, biashara ya vipodozi kupitia Instagram na WhatsApp ndiyo imekuwa mkombozi wake baada ya kukosa kazi kwa muda mrefu.

Neema ambaye ni mkazi wa Magomeni, Dar es Salaam anasema alianza kwa kuuza bidhaa chache kwa marafiki zake kupitia status za WhatsApp kabla ya kupata wateja wengi zaidi kupitia Instagram.

Anasema biashara za mtandaoni zimefungua milango kwa vijana wengi hasa wanawake ambao hawakuwa na uwezo wa kuanzisha biashara kubwa.

“Zamani ungehitaji duka, kodi na mtaji mkubwa. Sasa unaweza kuanza ukiwa nyumbani. Simu na intaneti vinatosha kama una ubunifu,” anasema Neema.

Hata hivyo, nyuma ya picha za mafanikio zinazoonekana mitandaoni, vijana hao wanasema safari ya kujijenga kidijitali si rahisi kama wengi wanavyodhani.

Mtengeneza maudhui ya YouTube, Abdul Ramadhani, anasema alitumia zaidi ya mwaka mmoja akitengeneza video bila kupata mapato yoyote ya maana.

“Kuna wakati unaweka video nzima halafu wanaotazama ni watu wawili tu. Watu wengi wanaona kama ni rahisi kupata fedha mtandaoni, lakini ukweli ni kwamba unahitaji uvumilivu mkubwa,” anasema Abdul.

Anasema changamoto kubwa ni ushindani mkubwa pamoja na mabadiliko ya mara kwa mara ya mifumo ya mitandao ambayo wakati mwingine hupunguza idadi ya watu wanaofikiwa na maudhui yao.

Kwa upande wake, Asha Khamis anayefanya biashara ya mavazi mtandaoni, anasema changamoto nyingine ni kukutana na wateja wasiokuwa waaminifu.

“Kuna wanaouliza bei na kuagiza lakini mwisho wa siku hawapokei simu wala kulipia mzigo. Biashara ya mtandaoni inahitaji subira sana,” anasema Asha.

Pamoja na changamoto hizo, vijana wengi wanaendelea kuona teknolojia kama tumaini jipya la maisha yao.

Juma Makala ambaye kazi yake ni kusambaza na kuuza bidhaa za wafanyabiashara kupitia mitandao ya kijamii maarufu kama “winga”, anasema biashara hiyo imemwezesha kujitegemea bila kusubiri ajira ya kuajiriwa.

“Ukiwa mvivu hupati kitu. Lazima ujitume muda wote, uwe mbunifu na ujue kuwashawishi watu kununua bidhaa,” anasema Juma.

Wasemavyo wachumi

Kwa mujibu wa wataalamu wa uchumi, ongezeko la vijana wanaoingia katika uchumi wa kidijitali linaonyesha namna mfumo wa ajira unavyoendelea kubadilika duniani.

Akizungumzia hilo mtaalamu wa uchumi, Henry Moshi anasema zama ambazo ajira zilitegemea zaidi ofisi za kawaida zinaendelea kupungua huku teknolojia ikifungua fursa mpya kwa vijana.

Anasema kadiri matumizi ya teknolojia yanavyozidi kuongezeka nchini, ndivyo vijana wengi wanavyoendelea kuiona intaneti kama eneo jipya la kutafuta maisha.

“Mustakabali wa ajira unaelekea zaidi kwenye ubunifu, teknolojia na biashara za mtandaoni. Uchumi wa kidijitali unaweza kuwa suluhisho kubwa la tatizo la ajira kwa vijana iwapo utaungwa mkono vizuri,” anasema Moshi.

Hata hivyo, anatahadharisha wengi wanaingia kwenye sekta hiyo bila elimu ya fedha wala uelewa wa namna ya kuendesha biashara endelevu.

“Wapo wanaopata fedha nyingi ghafla lakini hawana uwezo wa kupanga matumizi au kuwekeza. Bila elimu ya fedha, wengine wanaweza kuanza vizuri lakini wakashindwa kudumu,” anasema Moshi.

Mchumi mwingine, Andrew Maricha anasema mitandao ya kijamii imekuwa soko kubwa la ajira kwa vijana lakini pia lina changamoto ya kutokuwa na uhakika wa muda mrefu.

“Leo unaweza kuwa na wafuatiliaji wengi na kipato kizuri, kesho algorithm (mpangilio wa app) ikabadilika ukapoteza kila kitu. Ndiyo maana vijana wanapaswa kuwa wabunifu muda wote,” anasema Maricha.

Kutokana na hilo, anashauri Serikali kuwekeza zaidi katika mafunzo ya ujasiriamali wa kidijitali pamoja na kuboresha upatikanaji wa intaneti nafuu ili kuwasaidia vijana wengi zaidi kunufaika na sekta hiyo.

Hoja hiyo inaungwa mkono na mchumi Rehema Mdoe anayesema vijana wengi bado hawana ujuzi wa kutosha wa kutumia teknolojia kwa tija.

“Mitandao ni chombo tu. Tatizo ni kwamba baadhi ya vijana hawajui kusoma masoko, kupanga biashara au kutumia data vizuri. Wakijengewa uwezo, hii inaweza kuwa sekta kubwa ya ajira,” anasema Mdoe.

Licha ya changamoto zilizopo, baadhi ya vijana wanaamini dunia ya kidijitali imefungua ukurasa mpya ambao haukuwepo miaka michache iliyopita.

Salma Rajab, Mtengeneza maudhui ya mitindo katika Instagram na TikTok, anasema ndoto yake ni kuwa na kampuni kubwa ya mavazi kupitia umaarufu wa mitandao ya kijamii.

“Nimeona watu wengi wakibadilisha maisha yao kupitia TikTok na Instagram. Hilo linanipa matumaini kwamba na mimi naweza kufika mbali,” anasema Salma.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *