
Dar es Salaam. Wakati vifo vya Ebola vikifikia 220, ikiwa ni ongezeko la watu 20 waliopoteza maisha ndani ya saa 24 zilizopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) limetahadharisha kasi ya kuenea kwa ugonjwa huo huku Kituo cha Kukinga na Kudhibiti Magonjwa (CDC) kikisema nchi 11 zipo kwenye hatari ya maambukizi.
Nchi hizo ni Angola, Burundi, Jamhuri ya Afrika ya Kati, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania, Zambia pamoja na Uganda ambayo maambukizi sasa yanaenea.
Onyo hilo limetolewa jana Jumatatu na Mkurugenzi Mkuu wa CDC Afrika, Dk Jean Kaseya, aliyesema hali ya sasa ni ya kutisha na inahitaji mshikamano wa haraka wa kimataifa ili kudhibiti ugonjwa huo.
“Hatuna uwezo wa kuendelea kushuhudia Waafrika wakifa. Huu ni mzigo mkubwa mno kwa bara letu,” amesema Dk Kaseya katika mkutano wa viongozi wa afya kutoka mataifa mbalimbali ya Afrika uliojadili hatua za kukabili mlipuko huo.
Kwa mujibu wa taarifa za mamlaka za afya, zaidi ya watu 900 wanashukiwa kuambukizwa Ebola katika maeneo mbalimbali ya mashariki mwa DRC, huku idadi ya waliokufa ikifikia 220.
Ugonjwa huo umeenea zaidi katika jimbo la Ituri, lakini tayari kesi zimeonekana pia katika majimbo ya Kivu Kaskazini na Kivu Kusini karibu na mpaka wa Rwanda.
Shirika la Afya Duniani, WHO limesema kasi ya maambukizi imekuwa kubwa kuliko uwezo wa sasa wa kudhibiti ugonjwa huo. Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Ghebreyesus amesema timu za afya “zinaendelea kuukimbiza mlipuko” baada ya kuchelewa kugundua visa vya awali.
“Kwa sasa mlipuko unatuzidi kasi,” amesema Dk Tedros, ambaye ametangaza safari ya kwenda DRC ili kuimarisha uratibu wa mapambano dhidi ya Ebola.
Sintofahamu yaibuka
Katika hatua nyingine, polisi mashariki mwa DRC walilazimika kufyatua risasi hewani kuwatawanya wananchi waliokuwa wamezingira kituo cha matibabu ya Ebola mjini Mongwalu wakitaka kuchukua miili ya ndugu zao waliofariki dunia.
Taarifa kutoka eneo hilo zinasema wananchi wenye hasira walitaka miili ya watu wawili waliodaiwa kufariki kwa Ebola irejeshwe kwa familia zao kwa ajili ya mazishi ya kawaida.
Madaktari na wataalamu wa afya wameonya kuwa miili ya watu waliokufa kwa Ebola huwa na maambukizi makubwa na inaweza kuongeza kasi ya kusambaa kwa virusi ikiwa haitazikwa kwa utaratibu maalumu wa kiafya.
Hofu, imani potofu na kutokuamini taarifa za Serikali zimeendelea kuwa changamoto kubwa katika mapambano dhidi ya Ebola mashariki mwa Congo. Wiki iliyopita, wananchi walichoma moto mahema ya kutenga wagonjwa katika mji wa Rwampara baada ya kuzuiwa kuchukua mwili wa mtu aliyeshukiwa kufa kwa Ebola.
Wakati huohuo, Uganda imethibitisha wagonjwa wawili wapya wa Ebola kwa wahudumu wa afya, na kufanya idadi ya maambukizi nchini humo kufikia saba huku mtu mmoja akifariki dunia.
Kutokana na hali hiyo, Africa CDC imetaja nchi 11 za Afrika kuwa katika hatari ya kuathirika na mlipuko huo.
Dk Kaseya amesema mawaziri wa afya kutoka DRC, Uganda na Sudan Kusini wamekubaliana mpango wa pamoja wa kukabiliana na mlipuko huo wenye bajeti ya dola milioni 319 za Marekani.
Kwa mujibu wake, asilimia 10 pekee ya fedha hizo ndiyo zimepatikana hadi sasa kutoka kwa nchi husika, huku juhudi za kutafuta msaada zaidi zikiendelea.
Rais wa South Africa, Cyril Ramaphosa, ametangaza msaada wa awali wa dola milioni tano kusaidia mapambano dhidi ya Ebola na kuzitaka nchi nyingine za Afrika kuungana katika juhudi hizo.
“Afrika haiwezi kuendelea kusubiri mataifa mengine kuchukua hatua kwanza. Usalama wa dunia unaanza na usalama wa Afrika,” amesema Ramaphosa.
WHO pia imetangaza mlipuko huo kuwa dharura ya afya ya kimataifa kutokana na hatari ya kusambaa kwa ugonjwa huo katika mipaka ya nchi mbalimbali.
Mlipuko wa sasa unasababishwa na aina adimu ya virusi vya Bundibugyo Ebola ambayo haijaonekana kwa zaidi ya miaka 10. Wataalamu wanasema changamoto kubwa ni kwamba hadi sasa hakuna chanjo wala dawa maalumu iliyothibitishwa kufanya kazi dhidi ya aina hiyo ya Ebola.
WHO imeonya kuwa inaweza kuchukua hadi miezi tisa kupata chanjo inayoweza kutumika dhidi ya virusi hivyo, hali inayoongeza hofu ya kuendelea kuongezeka kwa maambukizi na vifo katika eneo la Afrika Mashariki na Kati.
